Mark (8/16)  

1. Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia,
2. Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula;
3. nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali.
4. Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani?
5. Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba,
6. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; wakawaandikia mkutano.
7. Walikuwa na visamaki vichache; akavibarikia, akasema wawaandikie na hivyo pia.
8. Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba.
9. Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga.
10. Mara akapanda chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.
11. Wakatokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana naye; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu.
12. Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki.
13. Akawaacha, akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng'ambo.
14. Wakasahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu.
15. Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.
16. Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate.
17. Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito?
18. Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki?
19. Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili.
20. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba.
21. Akawaambia, Hamjafahamu bado?
22. Wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse.
23. Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu?
24. Akatazama juu, akasema, Naona watu kama miti, inakwenda.
25. Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi.
26. Akampeleka nyumbani kwake, akisema, Hata kijijini usiingie.
27. Akatoka Yesu na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani?
28. Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii.
29. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo.
30. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake.
31. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.
32. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea.
33. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.
34. Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.
35. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.
36. Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
37. Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?
38. Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.

  Mark (8/16)