Mark (6/16)  

1. Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata.
2. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?
3. Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.
4. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.
5. Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya.
6. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao. Akazunguka-zunguka katika vile vijiji, akifundisha.
7. Akawaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu;
8. akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni;
9. lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili.
10. Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale.
11. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao.
12. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu.
13. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.
14. Naye Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake.
15. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii.
16. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka.
17. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa;
18. kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo.
19. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate.
20. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha.
21. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya;
22. ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa.
23. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.
24. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji.
25. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.
26. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia.
27. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani,
28. akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye.
29. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
30. Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha.
31. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula.
32. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu.
33. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika.
34. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35. Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa;
36. uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula.
37. Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula?
38. Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili.
39. Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi.
40. Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini.
41. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote.
42. Wakala wote wakashiba.
43. Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia.
44. Na walioila ile mikate wapata elfu tano wanaume.
45. Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng'ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.
46. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba.
47. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu.
48. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita.
49. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe,
50. kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope.
51. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao;
52. kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito.
53. Hata walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti, wakatia nanga.
54. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua,
55. wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo.
56. Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.

  Mark (6/16)