| ← Mark (16/16) |
| 1. | Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka. |
| 2. | Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza; |
| 3. | wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi? |
| 4. | Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno. |
| 5. | Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu. |
| 6. | Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. |
| 7. | Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia. |
| 8. | Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa. [ |
| 9. | Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba. |
| 10. | Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia. |
| 11. | Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki. |
| 12. | Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba. |
| 13. | Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki. |
| 14. | Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. |
| 15. | Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. |
| 16. | Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. |
| 17. | Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; |
| 18. | watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. |
| 19. | Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. |
| 20. | Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.] |
| ← Mark (16/16) |