| ← Mark (15/16) → |
| 1. | Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato. |
| 2. | Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema. |
| 3. | Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. |
| 4. | Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! |
| 5. | Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu. |
| 6. | Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye. |
| 7. | Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, amefungwa pamoja na watu waliofanya fitina, na kufanya uuaji katika fitina ile. |
| 8. | Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea. |
| 9. | Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi? |
| 10. | Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda. |
| 11. | Lakini wakuu wa makuhani wakawataharakisha makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba. |
| 12. | Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi? |
| 13. | Wakapiga kelele tena, Msulibishe. |
| 14. | Pilato akawaambia, Kwani, ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulibishe. |
| 15. | Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe. |
| 16. | Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima. |
| 17. | Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani; |
| 18. | wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! |
| 19. | Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia. |
| 20. | Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe. |
| 21. | Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake. |
| 22. | Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa. |
| 23. | Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee. |
| 24. | Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini. |
| 25. | Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha. |
| 26. | Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI. |
| 27. | Na pamoja naye walisulibisha wanyang'anyi wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. [ |
| 28. | Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.] |
| 29. | Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, |
| 30. | jiponye nafsi yako, ushuke msalabani. |
| 31. | Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe. |
| 32. | Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea. |
| 33. | Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. |
| 34. | Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? |
| 35. | Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. |
| 36. | Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha. |
| 37. | Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. |
| 38. | Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini. |
| 39. | Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. |
| 40. | Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; |
| 41. | hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu. |
| 42. | Hata ikiisha kuwa jioni, kwa sababu ni Maandalio, ndiyo siku iliyo kabla ya sabato, |
| 43. | akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu. |
| 44. | Lakini Pilato akastaajabu, kwamba amekwisha kufa. Akamwita yule akida, akamwuliza kwamba amekufa kitambo. |
| 45. | Hata alipokwisha kupata hakika kwa yule akida, alimpa Yusufu yule maiti. |
| 46. | Naye akanunua sanda ya kitani, akamtelemsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi. |
| 47. | Nao Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose wakapatazama mahali alipowekwa. |
| ← Mark (15/16) → |