← Mark (14/16) → |
1. | Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua. |
2. | Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu. |
3. | Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake. |
4. | Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii? |
5. | Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung'unikia sana yule mwanamke. |
6. | Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema; |
7. | maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote. |
8. | Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. |
9. | Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake. |
10. | Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. |
11. | Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa. |
12. | Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka? |
13. | Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni; |
14. | na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? |
15. | Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni. |
16. | Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. |
17. | Basi ilipokuwa jioni yuaja pamoja na wale Thenashara. |
18. | Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti. |
19. | Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi? |
20. | Akawaambia, Ni mmoja wa hao Thenashara, ambaye achovya pamoja nami katika kombe. |
21. | Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. |
22. | Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu. |
23. | Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. |
24. | Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. |
25. | Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu. |
26. | Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni. |
27. | Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. |
28. | Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. |
29. | Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. |
30. | Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. |
31. | Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile. |
32. | Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo. |
33. | Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. |
34. | Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. |
35. | Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. |
36. | Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. |
37. | Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? |
38. | Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. |
39. | Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. |
40. | Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. |
41. | Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. |
42. | Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia. |
43. | Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee. |
44. | Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama. |
45. | Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu. |
46. | Wakanyosha mikono yao wakamkamata. |
47. | Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. |
48. | Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang'anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi? |
49. | Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia. |
50. | Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote. |
51. | Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; |
52. | naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi. |
53. | Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi. |
54. | Naye Petro akamfuata kwa mbali, hata ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, anakota moto mwangani. |
55. | Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. |
56. | Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana. |
57. | Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, |
58. | Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. |
59. | Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana. |
60. | Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? |
61. | Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? |
62. | Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni. |
63. | Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? |
64. | Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa. |
65. | Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi. |
66. | Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu, |
67. | akamwona Petro akikota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu. |
68. | Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hata ukumbini; jogoo akawika. |
69. | Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao. |
70. | Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe. |
71. | Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena. |
72. | Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia. |
← Mark (14/16) → |