← Mark (13/16) → |
1. | Hata alipokuwa akitoka hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, Mwalimu, tazama, yalivyo mawe na majengo haya! |
2. | Yesu akajibu, akamwambia, Wayaona majengo haya makubwa? Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa. |
3. | Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, kuelekea hekalu Petro, na Yakobo, na Yohana, na Andrea walimwuliza kwa faragha, |
4. | Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya wakati, hayo yote yatakapokuwa karibu kutimia? |
5. | Yesu akaanza kuwaambia, Jihadharini, mtu asiwadanganye. |
6. | Wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye, nao watadanganya wengi. |
7. | Nanyi mtakaposikia habari za vita na uvumi wa vita, msitishwe; hayo hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado. |
8. | Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko ya nchi mahali mahali; kutakuwako na njaa; hayo ndiyo mwanzo wa utungu. |
9. | Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao. |
10. | Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote. |
11. | Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu. |
12. | Na ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, na baba atamsaliti mtoto, na watoto watashambulia wazazi wao, na kuwafisha. |
13. | Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kusaburi hata mwisho, ndiye atakayeokoka. |
14. | Lakini mlionapo chukizo la uharibifu likisimama pasipolipasa, (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; |
15. | na mtu aliye juu ya dari asishuke, wala asiingie kuchukua kitu nyumbani mwake; |
16. | naye aliye shambani asirudi nyuma kulichukua vazi lake. |
17. | Lakini ole wao wenye mimba, nao wanyonyeshao siku hizo! |
18. | Ila ombeni yasitokee hayo wakati wa baridi. |
19. | Kwa maana siku hizo zitakuwa na dhiki, jinsi isivyokuwa tangu mwanzo wa kuumba alipoumba Mungu hata sasa, wala haitakuwa kamwe. |
20. | Na kama Bwana asingalizikatiza siku hizo, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule aliowateua amezikatiza siku hizo. |
21. | Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki; |
22. | kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule. |
23. | Bali ninyi jihadharini; nimekwisha kuwaonya yote mbele. |
24. | Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hatautoa mwanga wake. |
25. | na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. |
26. | Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. |
27. | Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu. |
28. | Kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake liishapo kuwa laini, na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno ni karibu; |
29. | nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yanaanza, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni. |
30. | Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatimie. |
31. | Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. |
32. | Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba. |
33. | Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo. |
34. | Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe. |
35. | Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi; |
36. | asije akawasili ghafula akawakuta mmelala. |
37. | Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni. |
← Mark (13/16) → |