← Mark (11/16) → |
1. | Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake, |
2. | akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwana-punda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. |
3. | Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa. |
4. | Wakaenda zao, wakamwona mwana-punda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua. |
5. | Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwana-punda? |
6. | Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu. |
7. | Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake. |
8. | Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani. |
9. | Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; |
10. | umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni. |
11. | Naye akaingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara. |
12. | Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. |
13. | Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. |
14. | Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. |
15. | Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; |
16. | wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. |
17. | Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. |
18. | Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake. |
19. | Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. |
20. | Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. |
21. | Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. |
22. | Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. |
23. | Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. |
24. | Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. |
25. | Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. |
26. | Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.] |
27. | Wakafika Yerusalemu tena; hata alipokuwa akitembea hekaluni, walimwendea wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee, |
28. | wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya? |
29. | Yesu akawaambia, Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya. |
30. | Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni. |
31. | Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini? |
32. | Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, -- waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohana kuwa nabii halisi. |
33. | Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya. |
← Mark (11/16) → |