← Mark (10/16) → |
1. | Akaondoka huko akafika mipakani mwa Uyahudi, na ng'ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea. |
2. | Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. |
3. | Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? |
4. | Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. |
5. | Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. |
6. | Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. |
7. | Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; |
8. | na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. |
9. | Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. |
10. | Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. |
11. | Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; |
12. | na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini. |
13. | Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. |
14. | Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. |
15. | Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. |
16. | Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia. |
17. | Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? |
18. | Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. |
19. | Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. |
20. | Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. |
21. | Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. |
22. | Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. |
23. | Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! |
24. | Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! |
25. | Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. |
26. | Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? |
27. | Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu. |
28. | Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. |
29. | Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, |
30. | ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. |
31. | Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza. |
32. | Nao walikuwako njiani, huku wakipanda kwenda Yerusalemu; na Yesu alikuwa akiwatangulia, wakashangaa, nao katika kufuata wakaogopa. Akawatwaa tena wale Thenashara, akaanza kuwaambia habari za mambo yatakayompata, |
33. | akisema, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi, nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa, |
34. | nao watamdhihaki, na kumtemea mate, na kumpiga mijeledi, na kumwua; na baada ya siku tatu atafufuka. |
35. | Na Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba. |
36. | Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? |
37. | Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. |
38. | Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? |
39. | Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; |
40. | lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari. |
41. | Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana. |
42. | Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. |
43. | Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, |
44. | na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. |
45. | Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. |
46. | Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. |
47. | Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. |
48. | Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. |
49. | Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. |
50. | Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. |
51. | Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. |
52. | Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani. |
← Mark (10/16) → |