| Mark (1/16) → |
| 1. | Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. |
| 2. | Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako. |
| 3. | Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. |
| 4. | Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. |
| 5. | Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao. |
| 6. | Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu. |
| 7. | Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. |
| 8. | Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. |
| 9. | Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. |
| 10. | Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; |
| 11. | na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. |
| 12. | Mara Roho akamtoa aende nyikani. |
| 13. | Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. |
| 14. | Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, |
| 15. | akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. |
| 16. | Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. |
| 17. | Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. |
| 18. | Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. |
| 19. | Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. |
| 20. | Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata. |
| 21. | Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. |
| 22. | Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. |
| 23. | Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, |
| 24. | akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? |
| 25. | Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. |
| 26. | Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. |
| 27. | Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! |
| 28. | Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya. |
| 29. | Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. |
| 30. | Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. |
| 31. | Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. |
| 32. | Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. |
| 33. | Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. |
| 34. | Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. |
| 35. | Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. |
| 36. | Simoni na wenziwe wakamfuata; |
| 37. | nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. |
| 38. | Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea. |
| 39. | Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo. |
| 40. | Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. |
| 41. | Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. |
| 42. | Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. |
| 43. | Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, |
| 44. | akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. |
| 45. | Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali. |
| Mark (1/16) → |