Malachi (3/4)  

1. Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi.
2. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo;
3. naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki.
4. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
5. Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema Bwana wa majeshi.
6. Kwa kuwa mimi, Bwana, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo.
7. Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani?
8. Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.
9. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.
10. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.
11. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.
12. Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.
13. Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?
14. Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi?
15. Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.
16. Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake.
17. Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye.
18. Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia.

  Malachi (3/4)