Luke (7/24)  

1. Alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni mwa watu, aliingia Kapernaumu.
2. Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana.
3. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake.
4. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili;
5. maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi.
6. Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu;
7. kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona.
8. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.
9. Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii.
10. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.
11. Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa.
12. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.
13. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie.
14. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka.
15. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake.
16. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.
17. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.
18. Wanafunzi wa Yohana wakamletea habari za hayo yote.
19. Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?
20. Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?
21. Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona.
22. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema.
23. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.
24. Basi, wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo?
25. Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme.
26. Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii.
27. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.
28. Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.
29. Na watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana.
30. Lakini, Mafarisayo na wana-sheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye.
31. Bwana akasema, Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini?
32. Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.
33. Kwa kuwa Yohana Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai, nanyi mwasema, Ana pepo.
34. Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi.
35. Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.
36. Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake yule Farisayo, akaketi chakulani.
37. Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu.
38. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu.
39. Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.
40. Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena.
41. Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini.
42. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi?
43. Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki.
44. Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake.
45. Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu.
46. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu.
47. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.
48. Kisha alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako.
49. Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi?
50. Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani.

  Luke (7/24)