| ← Luke (4/24) → |
| 1. | Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, |
| 2. | akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. |
| 3. | Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. |
| 4. | Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. |
| 5. | Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. |
| 6. | Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. |
| 7. | Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. |
| 8. | Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. |
| 9. | Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; |
| 10. | kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; |
| 11. | na ya kwamba, |
| 12. | Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. |
| 13. | Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda. |
| 14. | Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. |
| 15. | Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. |
| 16. | Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. |
| 17. | Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, |
| 18. | Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, |
| 19. | Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. |
| 20. | Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. |
| 21. | Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. |
| 22. | Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? |
| 23. | Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe. |
| 24. | Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. |
| 25. | Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; |
| 26. | wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. |
| 27. | Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu. |
| 28. | Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. |
| 29. | Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; |
| 30. | lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake. |
| 31. | Akashuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya sabato; |
| 32. | wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo. |
| 33. | Na ndani ya sinagogi mlikuwa na mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu, |
| 34. | akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu. |
| 35. | Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno. |
| 36. | Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka. |
| 37. | Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile. |
| 38. | Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. |
| 39. | Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia. |
| 40. | Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. |
| 41. | Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. |
| 42. | Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. |
| 43. | Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. |
| 44. | Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya. |
| ← Luke (4/24) → |