| ← Luke (24/24) | 
| 1. | Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. | 
| 2. | Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi, | 
| 3. | Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu. | 
| 4. | Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta; | 
| 5. | nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? | 
| 6. | Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya, | 
| 7. | akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya tatu. | 
| 8. | Wakayakumbuka maneno yake. | 
| 9. | Wakaondoka kaburini, wakarudi; wakawaarifu wale kumi na mmoja na wengine wote habari za mambo hayo yote. | 
| 10. | Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine waliokuwa pamoja nao; | 
| 11. | hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo. | 
| 12. | Maneno yao yakaonekana kuwa kama upuzi kwao, wala hawakuwasadiki. Lakini Petro aliondoka akaenda mbio hata kaburini, akainama akachungulia ndani, akaviona vile vitambaa vya sanda tu; akaenda zake akiyastaajabia yaliyotukia. | 
| 13. | Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. | 
| 14. | Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. | 
| 15. | Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. | 
| 16. | Macho yao yakafumbwa wasimtambue. | 
| 17. | Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. | 
| 18. | Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? | 
| 19. | Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; | 
| 20. | tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. | 
| 21. | Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; | 
| 22. | tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, | 
| 23. | wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. | 
| 24. | Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. | 
| 25. | Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! | 
| 26. | Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? | 
| 27. | Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. | 
| 28. | Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. | 
| 29. | Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. | 
| 30. | Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. | 
| 31. | Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. | 
| 32. | Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko? | 
| 33. | Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, | 
| 34. | wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni. | 
| 35. | Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate. | 
| 36. | Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu. | 
| 37. | Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. | 
| 38. | Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? | 
| 39. | Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. | 
| 40. | Na baada ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake. | 
| 41. | Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula cho chote hapa? | 
| 42. | Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. | 
| 43. | Akakitwaa, akala mbele yao. | 
| 44. | Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi. | 
| 45. | Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. | 
| 46. | Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; | 
| 47. | na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. | 
| 48. | Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. | 
| 49. | Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. | 
| 50. | Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki. | 
| 51. | Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni. | 
| 52. | Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. | 
| 53. | Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu. | 
| ← Luke (24/24) |