| ← Luke (23/24) → |
| 1. | Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato. |
| 2. | Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. |
| 3. | Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. |
| 4. | Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu. |
| 5. | Nao walikaza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote, tokea Galilaya mpaka huku. |
| 6. | Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya. |
| 7. | Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile. |
| 8. | Na Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akataraji kuona ishara iliyofanywa na yeye. |
| 9. | Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lo lote. |
| 10. | Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. |
| 11. | Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. |
| 12. | Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao. |
| 13. | Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu, |
| 14. | akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; |
| 15. | wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilolitenda lipasalo kufa. |
| 16. | Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [ |
| 17. | Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.] |
| 18. | Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba. |
| 19. | Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji |
| 20. | Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu. |
| 21. | Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe. |
| 22. | Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua. |
| 23. | Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulibiwe. Sauti zao zikashinda. |
| 24. | Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. |
| 25. | Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo. |
| 26. | Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu. |
| 27. | Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. |
| 28. | Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. |
| 29. | Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. |
| 30. | Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. |
| 31. | Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu? |
| 32. | Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye. |
| 33. | Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. |
| 34. | Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. |
| 35. | Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. |
| 36. | Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, |
| 37. | huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. |
| 38. | Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. |
| 39. | Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. |
| 40. | Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? |
| 41. | Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. |
| 42. | Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. |
| 43. | Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. |
| 44. | Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, |
| 45. | jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. |
| 46. | Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. |
| 47. | Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki. |
| 48. | Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua. |
| 49. | Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo. |
| 50. | Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki; |
| 51. | (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu; |
| 52. | mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. |
| 53. | Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. |
| 54. | Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. |
| 55. | Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. |
| 56. | Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa. |
| ← Luke (23/24) → |