← Luke (20/24) → |
1. | Ikawa siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni, na kuihubiri habari njema, wakuu wa makuhani na waandishi pamoja na wazee walimtokea ghafula; |
2. | wakamwambia, wakisema, Tuambie, unatenda mambo hayo kwa mamlaka gani? Tena, ni nani aliyekupa mamlaka hii? |
3. | Akajibu akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja; niambieni, |
4. | Ubatizo wa Yohana, je! Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? |
5. | Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema ulitoka mbinguni, atasema, Basi, mbona hamkumwamini? |
6. | Na tukisema ulitoka kwa wanadamu, watu wote watatupiga kwa mawe, kwa kuwa wamemkubali Yohana kuwa ni nabii. |
7. | Wakajibu, kwamba, Hatujui ulikotoka. |
8. | Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya. |
9. | Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akapangisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu. |
10. | Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu. |
11. | Akatuma na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu. |
12. | Akamtuma na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje. |
13. | Basi, bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa wangu; yamkini watamheshimu yeye. |
14. | Lakini, wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu. |
15. | Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu atawatendeje? |
16. | Atakuja na kuwaangamiza wakulima wale, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Waliposikia hayo walisema, Hasha! Yasitukie haya! |
17. | Akawakazia macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni? |
18. | Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; na ye yote ambaye litamwangukia litamsaga kabisa. |
19. | Nao waandishi na wakuu wa makuhani walitafuta kumkamata saa iyo hiyo, wakawaogopa watu, maana walitambua ya kwamba mfano huu amewanenea wao. |
20. | Wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. |
21. | Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli. |
22. | Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo? |
23. | Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia, |
24. | Nionyesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari. |
25. | Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu. |
26. | Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa. |
27. | Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza, |
28. | wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. |
29. | Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; |
30. | na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] |
31. | hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. |
32. | Mwisho akafa yule mke naye. |
33. | Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. |
34. | Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; |
35. | lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; |
36. | wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. |
37. | Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. |
38. | Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake. |
39. | Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema; |
40. | wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo. |
41. | Akawaambia, Wasemaje watu kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? |
42. | Maana, Daudi mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, |
43. | Hata niwaweke adui zako Kuwa kiti cha kuwekea miguu yako. |
44. | Basi Daudi amwita Bwana; amekuwaje mwana wake? |
45. | Na watu wote walipokuwa wakimsikiliza, aliwaambia wanafunzi wake, |
46. | Jilindeni na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele karamuni. |
47. | Wanakula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu. Hao watapata hukumu iliyo kuu. |
← Luke (20/24) → |