| ← Luke (2/24) → |
| 1. | Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. |
| 2. | Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. |
| 3. | Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. |
| 4. | Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; |
| 5. | ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. |
| 6. | Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, |
| 7. | akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. |
| 8. | Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. |
| 9. | Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. |
| 10. | Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; |
| 11. | maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. |
| 12. | Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. |
| 13. | Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, |
| 14. | Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. |
| 15. | Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. |
| 16. | Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. |
| 17. | Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. |
| 18. | Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. |
| 19. | Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. |
| 20. | Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa. |
| 21. | Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. |
| 22. | Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, |
| 23. | (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), |
| 24. | wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. |
| 25. | Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. |
| 26. | Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. |
| 27. | Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, |
| 28. | yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, |
| 29. | Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; |
| 30. | Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, |
| 31. | Uliouweka tayari machoni pa watu wote; |
| 32. | Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. |
| 33. | Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. |
| 34. | Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. |
| 35. | Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. |
| 36. | Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. |
| 37. | Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. |
| 38. | Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. |
| 39. | Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. |
| 40. | Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. |
| 41. | Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. |
| 42. | Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; |
| 43. | na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. |
| 44. | Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; |
| 45. | na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. |
| 46. | Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. |
| 47. | Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. |
| 48. | Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. |
| 49. | Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? |
| 50. | Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. |
| 51. | Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. |
| 52. | Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. |
| ← Luke (2/24) → |