| ← Luke (19/24) → | 
| 1. | Naye alipoingia Yeriko alipita katikati yake. | 
| 2. | Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. | 
| 3. | Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. | 
| 4. | Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. | 
| 5. | Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. | 
| 6. | Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. | 
| 7. | Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. | 
| 8. | Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. | 
| 9. | Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. | 
| 10. | Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. | 
| 11. | Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. | 
| 12. | Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. | 
| 13. | Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja. | 
| 14. | Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale. | 
| 15. | Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. | 
| 16. | Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. | 
| 17. | Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. | 
| 18. | Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida. | 
| 19. | Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. | 
| 20. | Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso. | 
| 21. | Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. | 
| 22. | Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; | 
| 23. | basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? | 
| 24. | Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. | 
| 25. | Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi. | 
| 26. | Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho. | 
| 27. | Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu. | 
| 28. | Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu. | 
| 29. | Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi, | 
| 30. | akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa. | 
| 31. | Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji. | 
| 32. | Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. | 
| 33. | Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda? | 
| 34. | Wakasema, Bwana ana haja naye. | 
| 35. | Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu. | 
| 36. | Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. | 
| 37. | Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, | 
| 38. | wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. | 
| 39. | Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. | 
| 40. | Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele. | 
| 41. | Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, | 
| 42. | akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. | 
| 43. | Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; | 
| 44. | watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako. | 
| 45. | Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, | 
| 46. | akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. | 
| 47. | Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; | 
| 48. | wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza. | 
| ← Luke (19/24) → |