| ← Luke (18/24) → | 
| 1. | Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. | 
| 2. | Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. | 
| 3. | Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. | 
| 4. | Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, | 
| 5. | lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. | 
| 6. | Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. | 
| 7. | Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? | 
| 8. | Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? | 
| 9. | Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. | 
| 10. | Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. | 
| 11. | Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. | 
| 12. | Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. | 
| 13. | Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. | 
| 14. | Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. | 
| 15. | Wakamletea na watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi walipoona waliwakemea. | 
| 16. | Bali Yesu akawaita waje kwake, akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao. | 
| 17. | Amin, nawaambia, Mtu ye yote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe. | 
| 18. | Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele? | 
| 19. | Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. | 
| 20. | Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. | 
| 21. | Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. | 
| 22. | Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. | 
| 23. | Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. | 
| 24. | Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! | 
| 25. | Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. | 
| 26. | Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? | 
| 27. | Akasema, Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu. | 
| 28. | Petro akasema, Tazama, sisi tumeviacha vitu vyetu vyote na kukufuata. | 
| 29. | Akawaambia, Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu, | 
| 30. | asiyepokea zaidi mara nyingi katika zamani hizi, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. | 
| 31. | Akawachukua wale Thenashara, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote yatatimizwa, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii. | 
| 32. | Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na kutemewa mate; | 
| 33. | nao watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka. | 
| 34. | Walakini hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa. | 
| 35. | Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; | 
| 36. | na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? | 
| 37. | Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. | 
| 38. | Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu. | 
| 39. | Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. | 
| 40. | Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, | 
| 41. | Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. | 
| 42. | Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. | 
| 43. | Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu. | 
| ← Luke (18/24) → |