| ← Luke (17/24) → |
| 1. | Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! |
| 2. | Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. |
| 3. | Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. |
| 4. | Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe. |
| 5. | Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. |
| 6. | Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii. |
| 7. | Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? |
| 8. | Je! Hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? |
| 9. | Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? |
| 10. | Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya. |
| 11. | Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. |
| 12. | Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, |
| 13. | wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! |
| 14. | Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. |
| 15. | Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; |
| 16. | akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. |
| 17. | Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? |
| 18. | Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? |
| 19. | Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa. |
| 20. | Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; |
| 21. | wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu. |
| 22. | Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. |
| 23. | Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; |
| 24. | kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. |
| 25. | Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki. |
| 26. | Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. |
| 27. | Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. |
| 28. | Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; |
| 29. | lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. |
| 30. | Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. |
| 31. | Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. |
| 32. | Mkumbukeni mkewe Lutu. |
| 33. | Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya. |
| 34. | Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. |
| 35. | Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. |
| 36. | Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.] |
| 37. | Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai. |
| ← Luke (17/24) → |