| ← Luke (11/24) → | 
| 1. | Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake. | 
| 2. | Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] | 
| 3. | Utupe siku kwa siku riziki yetu. | 
| 4. | Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu]. | 
| 5. | Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, | 
| 6. | kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; | 
| 7. | na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe? | 
| 8. | Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake. | 
| 9. | Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. | 
| 10. | Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. | 
| 11. | Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? | 
| 12. | Au akimwomba yai, atampa nge? | 
| 13. | Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao? | 
| 14. | Naye alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. | 
| 15. | Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. | 
| 16. | Wengine walimjaribu, wakimtaka ishara itokayo mbinguni. | 
| 17. | Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. | 
| 18. | Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. | 
| 19. | Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. | 
| 20. | Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. | 
| 21. | Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; | 
| 22. | lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. | 
| 23. | Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya. | 
| 24. | Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, | 
| 25. | Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. | 
| 26. | Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. | 
| 27. | Ikawa alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. | 
| 28. | Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika. | 
| 29. | Na makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. | 
| 30. | Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. | 
| 31. | Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka ncha za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. | 
| 32. | Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona. | 
| 33. | Hakuna mtu awashaye taa na kuiweka mahali palipositirika, au chini ya pishi; bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuuona mwanga. | 
| 34. | Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza. | 
| 35. | Angalia basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza. | 
| 36. | Basi kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na giza, mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa mwanga wake. | 
| 37. | Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. | 
| 38. | Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. | 
| 39. | Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu. | 
| 40. | Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? | 
| 41. | Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu. | 
| 42. | Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. | 
| 43. | Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. | 
| 44. | Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. | 
| 45. | Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. | 
| 46. | Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu. | 
| 47. | Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. | 
| 48. | Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. | 
| 49. | Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, | 
| 50. | ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; | 
| 51. | tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. | 
| 52. | Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. | 
| 53. | Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, | 
| 54. | wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake. | 
| ← Luke (11/24) → |