Leviticus (6/27)  

1. Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2. Mtu awaye yote akifanya dhambi, na kuasi juu ya Bwana, akamdanganya mwenziwe katika jambo la amana, au la mapatano, au la kunyang'anya, au kumwonea mwenziwe;
3. au kuzumbua kitu kilichopotea na kutenda la uongo juu yake, na kuapa kwa uongo; katika mambo hayo yote mojawapo atakalolitenda mtu, na kufanya dhambi kwalo;
4. ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang'anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea alichokizumbua yeye,
5. au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia.
6. Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa Bwana, ni kondoo mume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani;
7. na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.
8. Bwana akanena na Musa na kumwambia,
9. Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike.
10. Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu.
11. Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya marago hata mahali safi.
12. Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake.
13. Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.
14. Na amri ya hiyo sadaka ya unga ni hii; wana wa Haruni wataisongeza mbele za Bwana, mbele ya madhabahu.
15. Naye atatwaa konzi yake katika huo unga, katika huo unga mwembamba wa sadaka ya unga, na katika mafuta yake, na ubani wote ulio juu ya sadaka ya unga, kisha atauteketeza juu ya madhabahu kuwa harufu ya kupendeza, kuwa ukumbusho wake kwa Bwana.
16. Na unga uliosalia Haruni na wanawe wataula; utaliwa pasipo kutiwa chachu, katika mahali patakatifu; katika ua wa hema ya kukutania ndipo watakapoula.
17. Hautaokwa na chachu. Nimewapa kuwa sehemu yao katika matoleo yangu yasongezwayo kwa njia ya moto; ni kitu kitakatifu sana, kama hiyo sadaka ya dhambi, na kama hiyo sadaka ya hatia.
18. Kila mwana mume miongoni mwa wana wa Haruni atakula katika huo, kuwa ni haki yao milele katika vizazi vyenu, katika matoleo ya Bwana yasongezwayo kwa njia ya moto; mtu awaye yote atakayevigusa atakuwa ni mtakatifu
19. Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
20. Matoleo ya Haruni na wanawe watakayomtolea Bwana, katika siku atakayotiwa mafuta, ni haya; sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga daima, nusu yake asubuhi, na nusu yake jioni.
21. Utaandaliwa kaangoni pamoja na mafuta; ukisha kulowama utauleta ndani; utasongeza hiyo sadaka ya unga vipande vilivyookwa, iwe harufu ya kupendeza kwa Bwana.
22. Na huyo kuhani aliyetiwa mafuta badala yake katika hao wanawe ataisongeza; itateketezwa kabisa kwa Bwana kwa amri ya milele.
23. Tena kila sadaka ya unga ya kuhani itateketezwa kabisa; isiliwe.
24. Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
25. Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya hiyo sadaka ya dhambi ni hii; mahali hapo pachinjwapo sadaka ya kuteketezwa ndipo itakapochinjwa sadaka ya dhambi, mbele za Bwana; ni takatifu sana.
26. Huyo kuhani atakayeisongeza kwa ajili ya dhambi ndiye atakayeila; italiwa katika mahali patakatifu, katika ua wa hema ya kukutania.
27. Kila kitu kitakachoigusa nyama ya sadaka hiyo kitakuwa kitakatifu; tena itakapomwagika damu yake yo yote katika nguo yo yote, utaifua nguo hiyo iliyomwagiwa, katika mahali patakatifu.
28. Lakini hicho chombo cha udongo ambacho hiyo nyama ilipikwa ndani yake kitavunjwa; na kama ikipikwa katika chombo cha shaba, kitasuguliwa, na kuoshwa kwa maji.
29. Kila mwana mume miongoni mwa makuhani atakula katika hiyo; ni takatifu sana.
30. Wala haitaliwa sadaka ya dhambi yo yote, ambayo damu yake yo yote ililetwa ndani ya hema ya kukutania, ili kufanya upatanisho katika mahali patakatifu; itachomwa moto.

  Leviticus (6/27)