Leviticus (3/27)  

1. Na matoleo yake kwamba ni sadaka za amani; kwamba asongeza katika ng'ombe, mume au mke, atamtoa huyo aliye mkamilifu mbele ya Bwana.
2. Naye ataweka mkono wake kichwani mwake huyo aliyemtoa, na kumchinja mlangoni pa hema ya kukutania; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.
3. Naye atasongeza katika sadaka hiyo ya amani, dhabihu kwa Bwana itakayofanywa kwa njia ya moto; yaani, mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo juu ya matumbo,
4. na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno, na hicho kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo; hayo yote atayaondoa.
5. Na wana wa Haruni watayateketeza kwa moto juu ya madhabahu, juu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo katika kuni zilizo juu ya moto; ni dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana.
6. Na matoleo yake kwa sadaka za amani atakayomchinjia Bwana, kwamba ni katika kundi la kondoo; mume au mke, atamtoa huyo aliye mkamilifu.
7. Kama akimtoa mwana-kondoo kuwa matoleo yake, ndipo atakapomtolea Bwana;
8. naye ataweka mkono wake kichwani mwake huyo aliyemsongeza, na kumchinja mlangoni pa hema ya kukutania; na wana wa Haruni watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.
9. Naye atasongeza katika sadaka hiyo ya amani dhabihu kwa Bwana, itakayofanywa kwa njia ya moto; yaani, mafuta yake, na mkia wenye mafuta mzima, atauondoa kwa kuukata hapo karibu na mfupa wa maungoni; na mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo,
10. na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo; hayo yote atayaondoa.
11. Naye kuhani atayateketeza kwa moto juu ya madhabahu; ni chakula cha dhabihu ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
12. Na matoleo yake, kwamba ni mbuzi, ndipo atakapomtoa mbele za Bwana;
13. naye ataweka mkono wake kichwani mwake, na kumchinja hapo mbele ya hema ya kukutania; na wana wa Haruni watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.
14. Naye atasongeza katika sadaka hiyo matoleo yake, dhabihu kwa Bwana kwa njia ya moto; yaani, mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo,
15. na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini pamoja na hizo figo mbili; hayo yote atayaondoa.
16. Naye kuhani atayateketeza kwa moto juu ya madhabahu; ni chakula cha dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, iwe harufu ya kupendeza; mafuta yote ni ya Bwana.
17. Neno hili litakuwa amri ya daima, katika vizazi vyenu vyote, ndani ya nyumba zenu zote, ya kwamba hamtakula mafuta wala damu kabisa.

  Leviticus (3/27)