Leviticus (26/27)  

1. Msifanye sanamu yo yote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara, wala msiweke jiwe lo lote lililochorwa katika nchi yenu ili kulisujudia; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
2. Zishikeni Sabato zangu, na kupastahi patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana.
3. Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya;
4. ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.
5. Tena kupura nafaka kwenu kutaendelea hata wakati wa kuvuna zabibu, na kuvuna zabibu kutaendelea hata wakati wa kupanda mbegu; nanyi mtakula chakula chenu na kushiba, na kuketi katika nchi yenu salama.
6. Nami nitawapa amani katika nchi, tena mtalala wala hapana atakayewatia hofu; nami nitawakomesha wanyama wabaya katika nchi yenu, wala hautapita upanga katika nchi yenu.
7. Nanyi mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga.
8. Na watu watano wa kwenu watawafukuza watu mia, na watu mia wa kwenu watawafukuza watu elfu kumi; na adui zenu wataanguka mbele yenu kwa upanga.
9. Nami nitawaelekezea uso wangu, na kuwapa uzazi mwingi, na kuwaongeza; nami nitalithibitisha agano langu pamoja nanyi.
10. Nanyi mtakula akiba ya zamani mliyoiweka siku nyingi, tena hayo ya zamani mtayatoa, ili myaweke yaliyo mapya.
11. Nami nitaiweka maskani yangu kati yenu; wala roho yangu haitawachukia.
12. Nami nitakwenda kati yenu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu.
13. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewaleta mtoke katika nchi ya Misri, ili msiwe watumwa wao; nami nimeivunja miti ya kongwa lenu, nikawaendesha mwende sawasawa.
14. Lakini msiponisikiza, wala hamtaki kuyafanya maagizo hayo yote;
15. nanyi mkizikataa amri zangu, na roho yenu ikichukia hukumu zangu, hata ikawa hamtaki kuyafanya maagizo yangu yote, bali mwalivunja agano langu;
16. mimi nami nitawatenda jambo hili; nitaamrisha uje juu yenu utisho, hata kifua kikuu na homa, zitakazoharibu macho yenu, na kuidhoofisha roho; nanyi mtapanda mbegu yenu bure, kwa kuwa adui zenu wataila.
17. Nami nitauelekeza uso wangu kinyume chenu, nanyi mtapigwa mbele ya adui zenu; hao wawachukiao watatawala juu yenu; nanyi mtakimbia wakati ambao hapana awafukuzaye.
18. Tena ikiwa baada ya hayo hamtaki kunisikiza, ndipo nitawaadhibu zaidi mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.
19. Nami nitakivunja kiburi cha uwezo wenu; nami nitazifanya mbingu zenu kuwa kama chuma, na nchi yenu kuwa kama shaba;
20. na nguvu zenu mtazitumia bure; kwa kuwa nchi yenu haitazaa mazao yake, wala miti ya nchi haitazaa matunda yake.
21. Nanyi ikiwa mwaenenda kinyume changu, wala hamtaki kunisikiza; nitaleta mapigo mara saba zaidi juu yenu, kama dhambi zenu zilivyo.
22. Nami nitaleta wanyama wakali kati yenu, ambao watawanyang'anya watoto wenu, na kuwaharibu wanyama wenu wa kufugwa, na kuwapunguza muwe wachache hesabu yenu; na njia zenu zitakuwa ni ukiwa.
23. Tena kama hamtaki kurejezwa upya kwangu mimi kwa mambo haya, bali mwaendelea kunishikia kinyume; ndipo mimi nami nitaendelea kuwashikia ninyi kinyume;
24. nami nitawapiga, naam mimi, mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.
25. Nami nitaleta upanga juu yenu, utakaopatiliza kisasi cha hilo agano; nanyi mtakutanishwa ndani ya miji yenu; nami nitaleta tauni kati yenu; nanyi mtatiwa mkononi mwa adui.
26. Hapo nitakapovunja tegemeo lenu la mkate, wanawake kumi wataoka mikate yenu katika tanuu moja, nao watawapa mikate yenu tena kwa kupima kwa mizani; nanyi mtakula, lakini hamtashiba.
27. Tena ikiwa baada ya hayo yote hamtaki kunisikiza, bali mwaenenda kwa kunishikia kinyume;
28. ndipo nami nitakwenda kwa kuwashikia ninyi kinyume katika ghadhabu yangu; nami nitawaadhibu mara saba kwa dhambi zenu.
29. Nanyi mtakula nyama ya miili ya wana wenu, na nyama ya miili ya binti zenu mtaila.
30. Nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka, na kuziangusha sanamu zenu za jua, nami nitaitupa mizoga yenu juu ya mizoga ya sanamu zenu; na roho yangu itawachukia.
31. Nami nitaifanya miji yenu iwe maganjo, na mahali penu patakatifu nitapatia ukiwa; wala sitasikia harufu ya manukato yenu yapendezayo.
32. Nami nitaitia hiyo nchi ukiwa; na adui zenu watakaokaa huko wataistaajabia.
33. Nanyi nitawatapanya-tapanya katika mataifa, nami nitaufuta upanga nyuma yenu; na nchi yenu itakuwa ni ukiwa, na miji yenu maganjo.
34. Hapo ndipo nchi itakapozifurahia Sabato zake, wakati itakapokuwa hali ya ukiwa, nanyi mtakapokuwa katika nchi ya adui zenu; ndipo nchi itakapopumzika, na kuzifurahia Sabato zake.
35. Wakati wote itakapokuwa na ukiwa, itapumzika; ni hayo mapumziko ambayo haikuwa nayo katika Sabato zenu, hapo mlipokaa katika nchi hiyo.
36. Tena hao wa kwenu watakaobaki, nitawatilia woga mioyoni mwao, katika hizo nchi za adui zao; na sauti ya jani lililopeperushwa itawakimbiza; nao watakimbia, kama mtu akimbiavyo upanga; nao wataanguka hapo ambapo hapana afukuzaye.
37. Nao wataangukiana wenyewe kwa wenyewe, kama mbele ya upanga, hapo ambapo hapana afukuzaye; wala hamtakuwa na nguvu za kusimama mbele ya adui zenu.
38. Nanyi mtaangamia kati ya mataifa, na nchi ya adui zenu itawameza.
39. Na watu wa kwenu watakaobaki watafifia kwa ajili ya uovu wao, katika hizo nchi za adui zenu; tena watafifia kwa ajili ya uovu wa baba zao, pamoja nao.
40. Nao wataukiri uovu wao, na uovu wa baba zao, katika maasi yao waliyoasi juu yangu, tena ya kuwa kwa sababu wameendelea kunishikia kinyume,
41. mimi nami nimeendelea kuwashikia kinyume wao, na kuwatia katika nchi ya adui zao; lakini hapo, kama mioyo yao isiyokuwa tohara ikinyenyekea, nao wakubali adhabu ya uovu wao;
42. ndipo nitakapokumbuka agano langu pamoja na Yakobo, tena agano langu na Isaka, tena agano langu na Ibrahimu nitalikumbuka; nami nitaikumbuka nchi hiyo.
43. Nchi nayo itaachwa na wao, nayo itazifurahia Sabato zake, itakapokuwa ukiwa pasipokuwa na wao; nao wataikubali adhabu ya uovu wao; kwa sababu, naam, ni kwa sababu wamezikataa hukumu zangu, na roho zao zimezichukia amri zangu.
44. Lakini pamoja na hayo yote, watakapokuwa katika nchi ya adui zao, mimi, sitawatupa, wala sitawachukia, niwaangamize kabisa, na kulivunja agano langu pamoja nao; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao;
45. lakini kwa ajili yao nitalikumbuka agano la baba zao, niliowaleta watoke katika nchi ya Misri mbele ya macho ya mataifa, ili kwamba niwe Mungu wao; mimi ndimi Bwana.
46. Hizi ni amri na hukumu na sheria, Bwana alizozifanya kati ya yeye na hao wana wa Israeli katika huo mlima wa Sinai kwa mkono wa Musa.

  Leviticus (26/27)