← Leviticus (24/27) → |
1. | Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, |
2. | Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. |
3. | Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za Bwana daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu. |
4. | Atazitengeza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za Bwana daima. |
5. | Nawe utatwaa unga mwembamba, na kuoka mikate kumi na miwili ya huo unga; sehemu za kumi mbili za efa, zitakuwa katika mkate mmoja. |
6. | Nawe iweke mistari miwili, mikate sita kwa kila mstari, juu ya hiyo meza safi, mbele za Bwana. |
7. | Nawe utatia ubani safi juu ya kila mstari, ili uwe ukumbusho kwa hiyo mikate, sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa moto. |
8. | Kila siku ya Sabato ataipanga mbele za Bwana daima; ni kwa ajili ya wana wa Israeli, agano la milele. |
9. | Nayo itakuwa ya Haruni na wanawe; nao wataila katika mahali patakatifu; kwa sababu kwake ni takatifu sana katika sadaka zisongezwazo kwa Bwana kwa moto, kwa amri ya milele. |
10. | Ikawa mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, ambaye babaye alikuwa Mmisri, akatokea kati ya wana wa Israeli; na huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, na Mwisraeli mmoja, wakapigana pamoja ndani ya marago; |
11. | kisha huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli akalikufuru hilo Jina, na kuapiza; nao wakamleta kwa Musa. Na jina la mamaye alikuwa akiitwa Shelomithi, binti ya Dibri, wa kabila ya Dani. |
12. | Nao wakamtia kifungoni, ili wapate kuambiwa neno litakalotoka kinywani pa Bwana. |
13. | Na Bwana akasema na Musa, na kumwambia, |
14. | Mtoe huyo aliyeapiza nje ya marago; na wale wote waliomsikia na waweke mikono yao kichwani mwake, kisha mkutano wote na wamwue kwa kumpiga kwa mawe. |
15. | Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu awaye yote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake. |
16. | Na yeye atakayelikufuru jina la Bwana hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzalia, hapo atakapolikufuru jina la Bwana atauawa. |
17. | Na mtu ampigaye mtu hata akafa, lazima atauawa; |
18. | na atakayempiga mnyama hata akafa atalipa; uhai kwa uhai. |
19. | Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo; |
20. | jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo. |
21. | Na mtu amwuaye mnyama atalipa; na yeye atakayemwua binadamu atauawa. |
22. | Mtakuwa na sheria moja tu, kwa huyo aliye mgeni, na kwa mzalia; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. |
23. | Musa akanena na wana wa Israeli, nao wakamtoa huyo aliyeapiza nje ya marago, wakamwua kwa kumpiga kwa mawe. Wana wa Israeli wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Musa. |
← Leviticus (24/27) → |