Leviticus (2/27)  

1. Na mtu atakapomtolea Bwana matoleo ya sadaka ya unga, matoleo yake yatakuwa ya unga mwembamba; naye ataumiminia mafuta, na kutia na ubani juu yake;
2. kisha atauleta kwa wana wa Haruni, hao makuhani; naye atatwaa konzi moja katika huo unga mwembamba, na katika mafuta yake, na huo ubani wote; kisha kuhani atauteketeza kuwa ndio ukumbusho wake juu ya madhabahu, ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana;
3. na huo uliosalia wa ile sadaka ya unga utakuwa ni wa Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
4. Tena, utakapotoa matoleo ya sadaka ya unga uliookwa tanuuni, yatakuwa mikate isiyotiwa chachu, ya unga mwembamba uliokandwa na mafuta, au maandazi yasiyochachwa yaliyopakwa mafuta.
5. Tena matoleo yako kwamba ni sadaka ya unga wa kaangoni, yatakuwa ya unga mwembamba usiotiwa chachu, uliokandwa na mafuta.
6. Utaukata-kata vipande, na kutia mafuta juu yake; ni sadaka ya unga.
7. Tena matoleo yako kwamba ni sadaka ya unga ya chunguni, yataandaliwa kwa unga mwembamba pamoja na mafuta.
8. Nawe utamletea Bwana sadaka ya unga iliyofanywa ya vitu hivyo; nayo italetwa kwa kuhani, naye ndiye atakayeisongeza madhabahuni.
9. Kisha kuhani atatwaa humo huo ukumbusho wa sadaka ya unga, naye atauteketeza juu ya madhabahu; ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.
10. Na hicho kitakachosalia katika sadaka ya unga kitakuwa cha Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
11. Sadaka ya unga iwayo yote itakayosongezwa kwa Bwana isitiwe chachu kabisa; kwa kuwa hamtateketeza chachu, wala asali iwayo yote, kuwa ni sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
12. Vitu hivyo mtavisongeza kwa Bwana kuwa ni malimbuko; lakini visifike juu ya madhabahu kuwa ni harufu ya kupendeza.
13. Tena, kila toleo la sadaka yako ya unga utalitia chumvi; wala usiiache sadaka yako ya unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na matoleo yako yote.
14. Nawe kwamba wamtolea Bwana sadaka ya unga ya malimbuko, utatoa hiyo ngano katika masuke yake iliyochomwa motoni, ngano iliyopondwa ya masuke mabichi, ndiyo utakayoleta kuwa sadaka ya unga ya malimbuko yako.
15. Nawe utatia mafuta juu yake, na kuweka ubani juu yake; ni sadaka ya unga.
16. Huyo kuhani atauteketeza ukumbusho wake, yaani, sehemu ya ngano iliyopondwa ya hiyo sadaka, na sehemu ya mafuta yake, pamoja na ule ubani wake wote; ni kafara ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.

  Leviticus (2/27)