← Leviticus (19/27) → |
1. | Bwana akanena na Musa, akamwambia, |
2. | Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu. |
3. | Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. |
4. | Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. |
5. | Nanyi hapo mtakapomchinjia Bwana sadaka ya amani mtaisongeza ili kwamba mpate kukubaliwa. |
6. | Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu cho chote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto. |
7. | Kwamba sadaka hiyo yaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa; |
8. | lakini kila mtu atakayekula atauchukua uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha Bwana; na nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. |
9. | Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako; |
10. | wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. |
11. | Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo. |
12. | Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. |
13. | Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang'anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi. |
14. | Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. |
15. | Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. |
16. | Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; mimi ndimi Bwana. |
17. | Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. |
18. | Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana. |
19. | Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja. |
20. | Tena mtu ye yote alalaye na mwanamke aliye mjakazi, naye ameposwa na mume, wala hakukombolewa kwa lo lote, wala hakupewa uhuru; wataadhibiwa; hawatauawa, kwa sababu huyo mwanamke hakuwa huru. |
21. | Na huyo mume ataleta sadaka yake ya hatia aitoe kwa Bwana, hata mlangoni pa hema ya kukutania; kondoo mume kwa hiyo sadaka ya hatia. |
22. | Kisha huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia mbele za Bwana, kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya. |
23. | Nanyi hapo mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama ni kutotahiriwa; muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa. |
24. | Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa Bwana shukrani. |
25. | Na katika mwaka wa tano mtakula katika matunda yake, ili ipate kuwapa maongeo yake; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. |
26. | Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi. |
27. | Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu. |
28. | Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana. |
29. | Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu. |
30. | Zishikeni Sabato zangu, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana. |
31. | Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. |
32. | Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi Bwana. |
33. | Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu. |
34. | Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. |
35. | Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani, wala katika cheo. |
36. | Mizani ya haki, vipimo vya haki, efa ya haki, hini ya haki, ndivyo mtakavyokuwa navyo. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri. |
37. | Zishikeni sheria zangu, na hukumu zangu, na kuzitenda. Mimi ndimi Bwana. |
← Leviticus (19/27) → |