| ← Leviticus (18/27) → | 
| 1. | Bwana akanena na Musa, na kumwambia, | 
| 2. | Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. | 
| 3. | Nanyi msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri mliyokaa; wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakayowapeleka; wala msiende katika amri zao hao. | 
| 4. | Mtazifanya hukumu zangu, nanyi mtazishika amri zangu, ili mwenende katika hizo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. | 
| 5. | Kwa ajili ya hayo mtazishika amri zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo; mimi ndimi Bwana. | 
| 6. | Mtu ye yote aliye wa kwenu asimkaribie mwenziwe aliye wa jamaa yake ya karibu ili kumfunua utupu; mimi ndimi Bwana. | 
| 7. | Utupu wa baba yako, wala utupu wa mama yako, usifunue, maana ndiye mama yako; usifunue utupu wake. | 
| 8. | Utupu wa mke wa baba yako, usifunue; maana, ni utupu wa baba yako. | 
| 9. | Utupu wa umbu lako, binti ya baba yako, au binti ya mama yako, kwamba alizaliwa nyumbani mwenu au kwamba alizaliwa kwengine, utupu wa hao usifunue. | 
| 10. | Utupu wa binti ya mwanao mume, au wa binti ya binti yako, utupu wao hao usifunue; kwa kuwa ndio utupu wako mwenyewe. | 
| 11. | Utupu wa binti ya mkewe baba yako, aliyezaliwa na baba yako, yeye ni umbu lako, usifunue utupu wake. | 
| 12. | Usifunue utupu wa umbu lake baba yako; maana, yeye ni jamaa aliye karibu. | 
| 13. | Usifunue utupu wa umbu la mama yako; maana, yeye ni jamaa ya mama yako ya karibu. | 
| 14. | Usifunue utupu wa ndugu ya baba yako, usimkaribie mkewe huyo; yeye ni shangazi lako. | 
| 15. | Usifunue utupu wa mkweo mwanamke; yeye ni mke wa mwanao; usifunue utupu wake huyo. | 
| 16. | Usifunue utupu wa mke wa nduguyo; maana, ni utupu wa nduguyo. | 
| 17. | Usifunue utupu wa mwanamke na binti yake; usimtwae binti ya mwanawe mume, au binti ya binti yake, ili kufunua utupu wake; hao ni jamaa ya karibu; ni uovu mkuu. | 
| 18. | Wala usitwae mwanamke pamoja na nduguye, awe mtesi wake, na kufunua utupu wake, huyo wa pili atakapokuwa yu hai. | 
| 19. | Nawe usimkaribie mwanamke kufunua utupu wake wakati wa kutengwa kwa ajili ya unajisi wake. | 
| 20. | Usilale na mke wa mwenzio, ukajitia unajisi naye. | 
| 21. | Nawe usitoe kizazi chako cho chote na kuwapisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi Bwana. | 
| 22. | Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo. | 
| 23. | Wala usilale na mnyama ye yote, ili kujitia unajisi kwake; wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala naye; ni uchafuko. | 
| 24. | Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; | 
| 25. | na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa. | 
| 26. | Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu; | 
| 27. | (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;) | 
| 28. | ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu. | 
| 29. | Kwani mtu awaye yote atakayefanya machukizo hayo mojawapo, nafsi hizo zitakazoyafanya zitakatiliwa mbali na watu wao. | 
| 30. | Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. | 
| ← Leviticus (18/27) → |