← Leviticus (15/27) → |
1. | Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, |
2. | Haya, semeni na wana wa Israeli, mkawaambie, Mtu ye yote atakapokuwa na kisonono kimtokacho mwilini mwake, atakuwa najisi kwa ajili ya kisonono chake. |
3. | Na unajisi wake katika kisonono chake ni huu; kama mwili wake unachuruzika kisonono chake, au kama kisonono chake kimezuiwa mwilini mwake, ni unajisi wake. |
4. | Kitanda cho chote akilaliacho mwenye kisonono kitakuwa najisi; na kitu cho chote ambacho akiketia kitakuwa najisi. |
5. | Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo, atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
6. | Na mtu atakayeketi katika kitu cho chote alichokiketia mwenye kisonono, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
7. | Na mtu atakayegusa mwili wake mwenye kisonono atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
8. | Tena kama mwenye kisonono akimtemea mate mtu aliye safi; ndipo atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa yu najisi hata jioni. |
9. | Na tandiko lo lote atakalolipanda mwenye kisonono litakuwa najisi. |
10. | Mtu awaye yote atakayegusa kitu cho chote kilichokuwa chini yake huyo atakuwa najisi hata jioni; na mtu atakayevichukua vitu vile atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
11. | Na mtu ye yote atakayeguswa na mwenye kisonono, asipokuwa amenawa mikono yake majini, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
12. | Na chombo cha udongo ambacho amekigusa mwenye kisonono, kitavunjwa-vunjwa; na kila chombo cha mti kitaoshwa majini. |
13. | Na huyo aliye na kisonono atakapotakaswa na kisonono chake, atajihesabia siku saba kwa kutakaswa kwake, naye atazifua nguo zake; naye ataoga mwili wake katika maji ya mtoni, naye atakuwa safi. |
14. | Na siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, naye atakwenda mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania, naye atampa kuhani hao ndege; |
15. | na kuhani atawasongeza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya kisonono chake. |
16. | Na mtu ye yote akitokwa na shahawa yake, ndipo ataoga mwili wake wote majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
17. | Na kila nguo, na kila ngozi, ambayo ina shahawa, itafuliwa kwa maji, nayo itakuwa najisi hata jioni. |
18. | Huyo mwanamke naye ambaye mtu mume amelala naye kwa shahawa, wote wawili wataoga majini, nao watakuwa najisi hata jioni. |
19. | Mwanamke ye yote, kama anatokwa na kitu, na kitu chake alichokuwa nacho mwilini mwake ni damu, ataketi katika kutengwa kwake muda wa siku saba; na mtu ye yote atakayemgusa atakuwa najisi hata jioni. |
20. | Na kitu cho chote akilaliacho katika kutengwa kwake kitakuwa najisi; na kila kitu ambacho akiketia kitakuwa najisi. |
21. | Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo mwanamke atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
22. | Mtu ye yote atakayekigusa cho chote ambacho huyo mwanamke amekiketia atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
23. | Kwamba ni katika kitanda, au cho chote alichokikalia huyo mwanamke, atakapokigusa kitu hicho, atakuwa najisi hata jioni. |
24. | Na mtu ye yote atakayelala na mwanamke na unajisi ukawa juu yake, atakuwa najisi muda wa siku saba; na kila kitanda alichokilalia kitakuwa najisi. |
25. | Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo si katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatoka damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutoka damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa katika siku za kutengwa kwake; yeye yu najisi. |
26. | Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake. |
27. | Na mtu ye yote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. |
28. | Lakini huyo mwanamke kwamba ametakaswa na kule kutoka damu kwake, ndipo atakapojihesabia siku saba, na baadaye atakuwa safi. |
29. | Siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania. |
30. | Kuhani atamsongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, kwa ajili ya kutoka damu ya unajisi kwake. |
31. | Ni hivi mtakavyowatenga wana wa Israeli na unajisi wao; ili wasife katika unajisi wao, hapo watakapoitia unajisi maskani yangu iliyo katikati yao. |
32. | Hii ndiyo sheria ya mwenye kisonono, na ya mtu ambaye shahawa yake yamtoka, akawa na unajisi kwa hiyo; |
33. | na ya mwanamke ambaye yu katika kutengwa kwake, na ya mtu ambaye ana kisonono, kama ni mtu mume, kama ni mtu mke, na ya huyo alalaye na mwanamke mwenye unajisi. |
← Leviticus (15/27) → |