Lamentations (5/5)    

1. Ee Bwana, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu.
2. Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri.
3. Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane.
4. Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa.
5. Watufuatiao wa juu ya shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote.
6. Tumewapa hao Wamisri mkono; Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.
7. Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.
8. Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.
9. Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani.
10. Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu; Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo.
11. Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni; Na mabikira katika miji ya Yuda.
12. Wakuu hutungikwa kwa mikono yao; Nyuso za wazee hazipewi heshima.
13. Vijana huyachukua mawe ya kusagia; Na watoto hujikwaa chini ya kuni.
14. Wazee wameacha kwenda langoni; Na vijana kwenda ngomani.
15. Furaha ya mioyo yetu imekoma; Machezo yetu yamegeuka maombolezo.
16. Taji ya kichwa chetu imeanguka; Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.
17. Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia; Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.
18. Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa, Mbweha hutembea juu yake.
19. Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.
20. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi?
21. Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.
22. Isipokuwa wewe umetukataa kabisa; Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.

  Lamentations (5/5)