| ← Lamentations (3/5) → |
| 1. | Mimi ni mtu aliyeona mateso Kwa fimbo ya ghadhabu yake. |
| 2. | Ameniongoza na kuniendesha katika giza Wala si katika nuru. |
| 3. | Hakika juu yangu augeuza mkono wake Mara kwa mara mchana wote. |
| 4. | Amechakaza nyama yangu na ngozi yangu; Ameivunja mifupa yangu. |
| 5. | Amejenga boma juu yangu, Na kunizungusha uchungu na uchovu. |
| 6. | Amenikalisha penye giza, Kama watu waliokufa zamani. |
| 7. | Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka; Ameufanya mnyororo wangu mzito. |
| 8. | Naam, nikilia na kuomba msaada, Huyapinga maombi yangu. |
| 9. | Ameziziba njia zangu kwa mawe yaliyochongwa; Ameyapotosha mapito yangu. |
| 10. | Alivyo kwangu ni kama dubu aoteaye, Kama simba aliye mafichoni. |
| 11. | Amezigeuza njia zangu, na kunirarua-rarua; Amenifanya ukiwa. |
| 12. | Ameupinda upinde wake, Na kunifanya niwe shabaha kwa mshale. |
| 13. | Amenichoma viuno Kwa mishale ya podo lake. |
| 14. | Nimekuwa dhihaka kwa watu wangu wote; Wimbo wao mchana kutwa. |
| 15. | Amenijaza uchungu, Amenikinaisha kwa pakanga. |
| 16. | Amenivunja meno kwa changarawe; Amenifunika majivu. |
| 17. | Umeniweka nafsi yangu mbali na amani; Nikasahau kufanikiwa. |
| 18. | Nikasema, Nguvu zangu zimepotea, Na tumaini langu kwa Bwana. |
| 19. | Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu, Pakanga na nyongo. |
| 20. | Nafsi yangu ikali ikiyakumbuka hayo, Nayo imeinama ndani yangu. |
| 21. | Najikumbusha neno hili, Kwa hiyo nina matumaini. |
| 22. | Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi. |
| 23. | Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu. |
| 24. | Bwana ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye. |
| 25. | Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo. |
| 26. | Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu. |
| 27. | Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake. |
| 28. | Na akae peke yake na kunyamaza kimya; Kwa sababu Bwana ameweka hayo juu yake. |
| 29. | Na atie kinywa chake mavumbini; Ikiwa yamkini liko tumaini. |
| 30. | Na amwelekezee yule ampigaye shavu lake; Ashibishwe mashutumu. |
| 31. | Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. |
| 32. | Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. |
| 33. | Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha. |
| 34. | Kuwaseta chini kwa miguu Wafungwa wote wa duniani, |
| 35. | Kuipotosha hukumu ya mtu Mbele zake Aliye juu, |
| 36. | Na kumnyima mtu haki yake, Hayo Bwana hayaridhii kabisa. |
| 37. | Ni nani asemaye neno nalo likafanyika, Ikiwa Bwana hakuliagiza? |
| 38. | Je! Katika kinywa chake Aliye juu Hayatoki maovu na mema? |
| 39. | Mbona anung'unika mwanadamu aliye hai Mtu akiadhibiwa kwa dhambi zake? |
| 40. | Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu, Na kumrudia Bwana tena. |
| 41. | Na tumwinulie Mungu aliye mbinguni Mioyo yetu na mikono. |
| 42. | Sisi tumekosa na kuasi; Wewe hukusamehe. |
| 43. | Umetufunika kwa hasira na kutufuatia; Umeua, wala hukuona huruma. |
| 44. | Umejifunika nafsi yako kwa wingu, Maombi yetu yasipite. |
| 45. | Umetufanya kuwa takataka, na vifusi Katikati ya mataifa. |
| 46. | Juu yetu adui zetu wote Wametupanulia vinywa vyao. |
| 47. | Hofu imetujilia na shimo, Ukiwa na uharibifu. |
| 48. | Jicho langu lachuruzika mito ya maji Kwa ajili ya uvunjifu wa binti ya watu wangu. |
| 49. | Jicho langu latoka machozi lisikome, Wala haliachi; |
| 50. | Hata Bwana atakapoangalia Na kutazama toka mbinguni. |
| 51. | Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu, Kwa sababu ya binti zote za mji wangu. |
| 52. | Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege; |
| 53. | Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani, Na kutupa jiwe juu yangu. |
| 54. | Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu, Nikasema, Nimekatiliwa mbali. |
| 55. | Naliliitia jina lako, Bwana, kutoka lile shimo Liendalo chini kabisa. |
| 56. | Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lako Ili usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu. |
| 57. | Ulinikaribia siku ile nilipokulilia; Ukasema, Usiogope. |
| 58. | Ee Bwana umenitetea mateto ya nafsi yangu; Umeukomboa uhai wangu. |
| 59. | Umekuona kudhulumiwa kwangu, Ee Bwana; Unihukumie neno langu. |
| 60. | Umekiona kisasi chao chote, Na mashauri yao yote juu yangu. |
| 61. | Ee Bwana, umeyasikia matukano yao, Na mashauri yao yote juu yangu; |
| 62. | Midomo yao walioinuka juu yangu Na maazimio yao juu yangu mchana kutwa. |
| 63. | Uangalie kuketi kwao, na kuinuka kwao; Wimbo wao ndio mimi. |
| 64. | Utawalipa malipo, Ee Bwana, Sawasawa na kazi ya mikono yao. |
| 65. | Utawapa ushupavu wa moyo; Laana yako juu yao. |
| 66. | Utawafuatia kwa hasira, na kuwaangamiza Wasiwe tena chini ya mbingu za Bwana. |
| ← Lamentations (3/5) → |