Judges (9/21)  

1. Abimeleki, mwana wa Yerubaali, akaenda Shekemu kwa ndugu za mama yake, akanena nao, na wote waliokuwa wa nyumba ya baba ya mama yake, akasema,
2. Haya, neneni tafadhali masikioni mwa waume wote wa Shekemu, mkaulize, Je! Ni lipi lililo jema kwenu, kwamba hao wana wa Yerubaali wote, ambao ni watu sabini, watawale juu yenu, au kwamba mtu mmoja atawale juu yenu? Tena kumbukeni ya kwamba mimi ni mfupa na nyama yenu.
3. Hao ndugu za mama yake wakanena habari zake masikioni mwa hao watu wote wa Shekemu maneno hayo yote; na mioyo yao ikaelekea kumwandama Abimeleki; kwa kuwa walisema, Huyu ni ndugu yetu.
4. Wakampa vipande vya fedha sabini vilivyotoka katika nyumba ya Baal-berithi, na kwa fedha hizo Abimeleki akaajiri watu wapuuzi mabaradhuli, wafuatane naye.
5. Kisha akaenda nyumbani kwa babaye huko Ofra, akawaua nduguze, hao wana wa Yerubaali, watu sabini, akawaua juu ya jiwe moja; lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubaali, alisalia; kwa maana alijificha.
6. Kisha hao watu wote wa Shekemu wakakusanyika pamoja, na jamaa yote ya Milo, wakaenda na kumtawaza Abimeleki awe mfalme, karibu na huo mgandi ulio karibu na ngome iliyo katika Shekemu.
7. Kisha walipomwambia huyo Yothamu, yeye akaenda, akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake, akapiga kelele, na kuwaambia, Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili kwamba Mungu naye apate kuwasikia ninyi.
8. Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu.
9. Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?
10. Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu.
11. Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti?
12. Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu.
13. Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?
14. Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo wewe, utawale juu yetu.
15. Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Kwamba ninyi mwanitia mafuta niwe mfalme juu yenu kwelikweli, basi njoni mtumaini kivuli changu; na kwamba sivyo, na utoke moto katika mti wa miiba na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni.
16. Basi sasa ikiwa mmetenda kwa uaminifu na uelekevu, katika kumtawaza Abimeleki awe mfalme, na ikiwa mmemtendea mema Yerubaali na nyumba yake, na kumtendea kama ilivyostahili mikono yake;
17. (kwa maana baba yangu aliwatetea ninyi, na kuhatirisha uhai wake, na kuwaokoa na mikono ya Midiani;
18. nanyi mmeinuka juu ya nyumba ya baba yangu hivi leo nanyi mmewaua wanawe, watu sabini, juu ya jiwe moja, nanyi mmemtawaza Abimeleki, mwana wa kijakazi chake, awe mfalme juu ya watu wa Shekemu kwa sababu yeye ni ndugu yenu;)
19. basi ikiwa mmemtendea kwa uaminifu na uelekevu Yerubaali na nyumba yake hivi leo, basi furahini ninyi katika huyo Abimeleki, yeye naye na afurahi kwenu ninyi;
20. lakini kwamba sivyo hivyo, basi, moto na utoke katika Abimeleki na kuwateketeza watu wa Shekemu, na jamaa ya Milo; kisha moto na utoke katika hao watu wa Shekemu, na katika jamaa ya Milo, na kumteketeza Abimeleki.
21. Kisha Yothamu akaenda zake na kukimbia, akaenda Beeri, na kukaa kuko, kwa kumwogopa Abimeleki nduguye.
22. Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli muda wa miaka mitatu.
23. Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu;
24. ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali uje, tena kwamba damu yao iandikwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze.
25. Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwanyang'anya vitu vyao watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliambiwa.
26. Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakamtumaini yeye.
27. Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki.
28. Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Yeye, je! Si mwana wa Yerubaali? Na Zebuli siye akida wake? Haya, ninyi watumikieni hao watu wa Hamori, babaye Shekemu; Lakini sisi je! Tumtumikie kwa sababu gani?
29. Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza askari zako, utoke nje.
30. Basi hapo Zebuli, aliyekuwa liwali wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka.
31. Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na tazama waufitinisha mji huu kinyume chako.
32. Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani;
33. kisha itakuwa, asubuhi, mara litakapokucha jua, wewe utaamka asubuhi na mapema, na kuushambulia mji huo; tena, angalia, hapo yeye na wale watu walio pamoja naye watakapokutokea nje kupigana nawe, ndipo utapata kuwatenda kama utakavyopata nafasi.
34. Basi Abimeleki akainuka na watu wote waliokuwa pamoja naye, usiku nao wakauvizia Shekemu kwa vikosi vinne.
35. Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia.
36. Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu.
37. Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu.
38. Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa ki wapi, hata ukasema Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio watu hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao.
39. Basi Gaali akatoka nje mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki.
40. Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi wakaanguka waliojeruhiwa hata kufikilia maingilio ya hilo lango.
41. Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu.
42. Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki aliambiwa.
43. Naye akawatwaa watu wake, na kuwagawanya wawe vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, na tazama, watu walikuwa watoka humo mjini; basi akainuka na kupigana nao, akawapiga.
44. Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafuliza kwenda mbele, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwapiga.
45. Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akaupomosha mji, na kuutia chumvi.
46. Kisha watu wote waliokaa katika ile buruji ya Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi.
47. Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa buruji ya Shekemu wamekutana pamoja.
48. Basi Abimeleki akakwea kwenda kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitweka fuzini mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, Haya, mliyoniona mimi kufanya, fanyeni upesi vivyo, kama nilivyofanya mimi.
49. Basi watu hao wote vivyo wakakata kila mtu tawi lake, wakamwandama Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; basi hivyo watu wote wa hiyo buruji ya Shekemu wakafa, walipata kama watu elfu, waume kwa wake.
50. Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akapanga kinyume cha Thebesi na kuutwaa.
51. Lakini ndani ya huo mji palikuwa na buruji yenye nguvu, na watu wote waume na wake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la buruji.
52. Abimeleki akaiendea hiyo buruji na kupigana nayo; naye akaukaribia mlango wa buruji ili auteketeze kwa moto.
53. Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake.
54. Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa.
55. Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake.
56. Basi hivyo Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, katika kuwaua hao nduguze watu sabini;
57. uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajilia juu yao.

  Judges (9/21)