Judges (7/21)  

1. Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni.
2. Bwana akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa.
3. Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu ishirini na mbili elfu wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi.
4. Bwana akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda.
5. Basi akawaleta watu chini majini. Bwana akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa.
6. Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji.
7. Bwana akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake.
8. Basi wale watu wakachukua vyakula vyao mikononi mwao, na tarumbeta zao; naye akawapeleka watu wote wa Israeli, kila mtu hemani kwake; bali aliwazuia wale watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni.
9. Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako.
10. Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini;
11. nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hata kufikilia mwisho wa watu wenye silaha waliokuwa kambini.
12. Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi.
13. Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini.
14. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake.
15. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana Bwana amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu.
16. Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi.
17. Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni kadhalika.
18. Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa Bwana, na kwa Gideoni.
19. Basi Gideoni, na wale watu mia waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao.
20. Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa Bwana na wa Gideoni.
21. Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza.
22. Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye Bwana akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi.
23. Wanaume wa Israeli walikuwa wamekusanyika kutoka Naftali, na kutoka Asheri, na kutoka Manase yote, wakawafuata Midiani.
24. Kisha Gideoni akapeleka wajumbe katika nchi yote ya vilima vilima ya Efraimu, akisema, Haya, telemkeni juu ya Midiani, na kuyashika hayo maji mbele yao, mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani. Basi watu waume wote wa Efraimu walikutana pamoja, wakayashika maji mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani.
25. Wakawashika hao wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu; wakamwua huyo Orebu pale penye jabali la Orebu, na huyo Zeebu wakamwua hapo penye shinikizo la divai la Zeebu, kisha wakawaandamia Wamidiani; vichwa vya Orebu na Zeebu wakamletea Gideoni huko ng'ambo ya pili ya Yordani.

  Judges (7/21)