Judges (5/21)  

1. Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema;
2. Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini Bwana.
3. Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu; Mimi, naam mimi, nitamwimbia Bwana; Nitamhimidi Bwana, Mungu wa Israeli.
4. Bwana, ulipotoka katika Seiri, Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu, Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondoza maji, Naam, mawingu yakadondoza maji.
5. Milima ikayeyuka mbele za uso wa Bwana, Naam hata Sinai ule mbele za uso wa Bwana, Mungu wa Israeli.
6. Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu; Nao wenye kusafiri walipita kwa njia za kando.
7. Maliwali walikoma katika Israeli, walikoma, Hata mimi Debora nilipoinuka, Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli.
8. Walichagua miungu mipya, Ndipo kulikuwa na vita malangoni; Je! Ilionekana ngao au mkuki Katika watu elfu arobaini wa Israeli?
9. Moyo wangu unawaelekea maliwali wa Israeli, Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu; Mhimidini Bwana.
10. Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe, Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani, Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu.
11. Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji, Hapo watatangaza matendo ya haki ya Bwana; Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli. Ndipo watu wa Bwana waliposhuka malangoni.
12. Amka, amka, Debora; Amka, amka, imba wimbo. Inuka, Baraka, wachukue mateka wao Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu.
13. Ndipo walitelemka mabaki ya waungwana na ya watu; Bwana alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa.
14. Kutoka Efraimu walitelemka wao ambao shina lao ni katika Amaleki, Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako. Kutoka Makiri walishuka maliwali, Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi.
15. Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora. Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka. Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake. Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
16. Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo, Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi? Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
17. Gileadi alikaa ng'ambo ya Yordani, Na Dani, mbona alikaa katika merikebu? Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari, Alikaa katika hori zake.
18. Zabuloni ndio watu waliohatirisha roho zao hata kufa; Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni.
19. Wafalme walikuja wakafanya vita, Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita. Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido; Hawakupata faida yo yote ya fedha.
20. Walipigana kutoka mbinguni, Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera.
21. Mto ule wa Kishoni uliwachukua, Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu.
22. Ndipo kwato za farasi zilikanyaga-kanyaga Kwa sababu ya kupara-para, Kupara-para kwao wenye nguvu.
23. Ulaanini Merozi, alisema malaika wa Bwana, Walaanini kwa uchungu wenyeji wake; Kwa maana hawakuja kumsaidia Bwana, Kumsaidia Bwana juu ya hao wenye nguvu.
24. Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote; Mkewe Heberi, Mkeni, Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani.
25. Aliomba maji, naye akampa maziwa. Akamletea siagi katika sahani ya heshima.
26. Akanyosha mkono wake akashika kigingi, Nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi; Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake. Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake.
27. Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala. Miguuni pake aliinama, akaanguka. Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa.
28. Alichungulia dirishani, akalia, Mama yake Sisera alilia dirishani; Mbona gari lake linakawia kufika? Mbona gurudumu za gari lake zinakawia?
29. Mabibi yake wenye akili wakamjibu, Naam, alijipa nafsi yake jawabu.
30. Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya, Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu? Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbali mbali, Nyara za mavazi ya rangi mbali mbali ya darizi; Ya rangi mbali mbali ya darizi, pande zote mbili, Juu ya shingo za hao mateka.
31. Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee Bwana.

  Judges (5/21)