Judges (3/21)  

1. Basi haya ndiyo mataifa ambao Bwana aliwaacha, ili awajaribu Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kanaani;
2. ili kwamba vizazi vya wana wa Israeli wapate kujua ili kuwafundisha vita, hasa wao ambao hawakujua vita kabla ya wakati ule;
3. aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti, na Wakanaani wote, na Wasidoni, na Wahivi waliokaa katika kilima cha Lebanoni, toka mlima wa Baal-hermoni mpaka kuingia Hamathi.
4. Naye aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao, apate kujua kwamba watasikiliza amri za Bwana, alizowaamuru baba zao, kwa mkono wa Musa.
5. Basi wana wa Israeli wakaketi kati ya Wakanaani; hao Wahiti, na hao Waamori, na hao Waperizi, na hao Wahivi na hao Wayebusi;
6. wakawaoa binti zao, na binti zao wenyewe wakawaoza wana wao waume, na kuitumikia miungu yao.
7. Wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakamsahau Bwana, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi.
8. Kwa hiyo hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane.
9. Kisha wana wa Israeli walipomlingana Bwana, Bwana akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.
10. Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.
11. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.
12. Basi wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu tena mbele za Bwana; naye Bwana akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli, kwa sababu walikuwa wameyafanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana.
13. Huyo Egloni akakutanisha kwake wana wa Amoni na Amaleki; akaenda na kuwapiga Israeli, nao wakauchukua huo mji wa mitende.
14. Wana wa Israeli walimtumikia Egloni mfalme wa Moabu muda wa miaka kumi na minane.
15. Lakini wana wa Israeli walipomlilia Bwana, Bwana akawainulia mwokozi, Ehudi, mwana wa Gera, Mbenyamini, mtu aliyekuwa mwenye shoto; nao wana wa Israeli walimpelekea Egloni mfalme wa Moabu tunu mkononi mwa huyo Ehudi.
16. Ehudi alijifanyia upanga uliokuwa na makali kuwili, urefu wake ulipata dhiraa moja; akaufunga huo upanga ndani ya nguo yake katika paja lake la mkono wa kuume.
17. Kisha akamsongezea Egloni, mfalme wa Moabu, hiyo tunu; basi Egloni alikuwa ni mtu aliyewanda sana.
18. Naye hapo alipokuwa amekwisha kuisongeza hiyo tunu, akawapa ruhusa watu hao walioichukua tunu, wakaenda zao.
19. Lakini yeye mwenyewe akageuka kutoka huko kwenye sanamu zilizokuwa karibu na Gilgali, akasema, Mimi nina ujumbe wa siri kwako wewe, Ee mfalme. Naye akasema, Nyamazeni kimya. Watu wote waliokuwa wanasimama karibu naye wakatoka na kumwacha.
20. Basi Ehudi akamwendea; naye alikuwa anaketi peke yake katika chumba chake cha baridi. Ehudi akasema, Mimi nina ujumbe utokao kwa Mungu kwako wewe. Basi akainuka katika kiti chake.
21. Ehudi akaunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kuume, akamtia tumboni mwake;
22. hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma.
23. Ndipo Ehudi akatoka nje barazani, akamfungia milango ya hicho chumba na kuifunga kwa ufunguo.
24. Basi alipokuwa amekwisha toka nje, hao watumishi wake wakaenda; wakaona, na tazama, hiyo milango ya chumba ilikuwa imefungwa kwa ufunguo; nao wakasema, Hapana budi amejifunika miguu yake ndani ya chumba cha baridi.
25. Wakangoja hata wakatahayari; na tazama, hakuifungua milango ya chumba; basi wakatwaa ufunguo, na kuifungua; na tazama, bwana wao alikuwa ameanguka nchi, naye amekufa.
26. Naye Ehudi alikimbia hapo walipokuwa wakingoja, akapita huko kwenye sanamu, na kukimbilia Seira.
27. Ikawa, hapo alipofika akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, ndipo wana wa Israeli wakatelemka pamoja naye kutoka huko milimani, naye akawatangulia.
28. Akawaambia, Niandameni mimi; kwa kuwa Bwana amewatia adui zenu, Wamoabi, mikononi mwenu. Basi wakatelemka na kumfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha Wamoabi, wala hawakumwacha mtu kuvuka.
29. Wakati huo wakapiga katika Wamoabi watu waume wapata kama elfu kumi, ambao wote walikuwa wanene, na wote mashujaa; hakupona hata mtu mmoja.
30. Basi Moabu alishindwa siku hiyo chini ya mikono ya Israeli. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka themanini
31. Tena baada yake huyo alikuwapo Shamgari mwana wa Anathi, aliyepiga katika Wafilisti watu mia sita kwa konzo la ng'ombe; yeye naye aliwaokoa Israeli.

  Judges (3/21)