← Judges (13/21) → |
1. | Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya Bwana, Bwana akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arobaini. |
2. | Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. |
3. | Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. |
4. | Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; |
5. | kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. |
6. | Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina lake; |
7. | lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake. |
8. | Ndipo huyo Manoa akamwomba Bwana, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa. |
9. | Mungu akasikiza sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye. |
10. | Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijilia siku ile. |
11. | Basi Manoa akainuka, akamwandama mkewe, na kumfikilia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Naam, ni mimi. |
12. | Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini? |
13. | Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari. |
14. | Asile kitu cho chote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu cho chote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze. |
15. | Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako. |
16. | Lakini malaika wa Bwana akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea Bwana. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa Bwana. |
17. | Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza? |
18. | Huyo malaika wa Bwana akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu? |
19. | Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea Bwana hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia. |
20. | Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa Bwana akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi. |
21. | Lakini malaika wa Bwana hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa Bwana. |
22. | Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu. |
23. | Lakini mkewe akamwambia, Kama Bwana angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu. |
24. | Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. |
25. | Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli. |
← Judges (13/21) → |