Joshua (10/24)  

1. Basi ikawa hapo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia jinsi Yoshua alivyoushika mji wa Ai na kuuharibu kabisa; kama alivyoufanyia mji wa Yeriko na mfalme wake, akaufanya vivyo Ai na mfalme wake; na jinsi wenyeji waliokaa Gibeoni walivyofanya amani na Israeli, na ya kwamba walikuwa kati yao;
2. ndipo wakacha mno, kwa sababu Gibeoni ulikuwa ni mji mkubwa, kama ilivyo miji ya kifalme mmojawapo, tena kwa sababu ulikuwa ni mji mkubwa kupita Ai, tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa.
3. Basi kwa hiyo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuthi, na kwa Yafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, akiwaambia,
4. Haya, kweeni mje kwangu, mnisaidie, tuupige Gibeoni; kwa sababu umefanya mapatano ya amani pamoja na Yoshua na wana wa Israeli.
5. Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni na mfalme wa Yarmuthi na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni, wakakutana pamoja, kisha wakakwea, wao na jeshi zao zote, na kupanga marago yao kinyume cha Gibeoni, na kuupiga vita.
6. Ndipo watu wa Gibeoni wakatuma wajumbe kwenda kwa Yoshua huko Gilgali maragoni, wakamwambia, Usiulegeze mkono wako hata ukatuacha sisi watumishi wako; uje kwetu kwa upesi, utuokoe, na kutusaidia; kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao katika nchi ya vilima wamekutana pamoja juu yetu.
7. Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wenye uwezo pia wote.
8. Bwana akamwambia Yoshua, Usiwache watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako.
9. Basi Yoshua akawafikilia ghafula; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha.
10. Bwana naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda.
11. Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Beth-horoni, ndipo Bwana alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga.
12. Ndipo Yoshua akanena na Bwana katika siku hiyo ambayo Bwana aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni.
13. Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao.
14. Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye Bwana kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa Bwana alipiga vita kwa ajili ya Israeli.
15. Basi Yoshua akarudi, na Israeli wote wakarudi pamoja naye, mpaka maragoni hapo Gilgali.
16. Na hawa wafalme watano wakakimbia, wakajificha ndani ya pango la Makeda.
17. Kisha Yoshua aliambiwa habari hiyo, ya kwamba, Hao wafalme watano wameonekana, nao wa hali ya kujificha ndani ya pango la Makeda
18. Basi Yoshua akasema, Haya, vingirisheni mawe makubwa mdomoni mwa lile pango, kisha wekeni watu hapo ili kuwalinda;
19. lakini msikae ninyi; wafuatieni adui zenu, mwapige hao walio nyuma; msiwaache wakaingia ndani ya miji yao; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu.
20. Kisha ikawa, hapo Yoshua, na wana wa Israeli, walipokuwa wamekwisha kuwaua watu wengi mno, hata wakaangamizwa, na hayo mabaki yao yaliyowasalia walipokuwa wamekwisha ingia katika miji yao yenye boma,
21. ndipo hao watu wote wakamrudia Yoshua maragoni huko Makeda salama; hakuna mtu awaye yote aliyetoa ulimi kinyume cha hao wana wa Israeli hata mmojawapo.
22. Kisha Yoshua akasema, Haya, funua mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano hapa nje ya pango.
23. Nao wakafanya, wakamletea hao wafalme watano hapo nje ya pango, yaani, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni, na mfalme wa Yarmuthi, na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni.
24. Kisha ikawa hapo walipomletea Yoshua hao wafalme watano hapo nje, Yoshua akawaita wanaume wote wa Israeli, akawaambia majemadari wa watu wa vita waliokwenda naye, Haya, jongeeni karibu, mweke nyayo za miguu yenu katika shingo za wafalme hawa. Nao wakajongea karibu, wakatia nyayo zao katika shingo zao.
25. Yoshua akawaambia, Msiche, wala msifadhaike; iweni hodari na wa mioyo ya ushujaa; kwa kuwa ndivyo Bwana atakavyowafanyia adui zenu wote ambao mwapigana nao.
26. Baadaye Yoshua akawapiga, na kuwaua, akawatundika katika miti mitano; nao wakawa wakitundikwa katika hiyo miti hata jioni.
27. Kisha wakati wa kuchwa jua, Yoshua akatoa amri, nao wakawatelemsha katika hiyo miti, na kuwatupa katika lile pango ambamo walikuwa walijificha kisha wakatia mawe makubwa mdomoni mwa pango, hata hivi leo.
28. Siku hiyo Yoshua akautwaa mji wa Makeda, akaupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake; akawaangamiza kabisa na wote pia waliokuwamo ndani yake, hakumwacha hata mmoja aliyesalia; naye akamfanyia huyo mfalme wa Makeda kama alivyomfanyia huyo mfalme wa Yeriko.
29. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Makeda, mpaka Libna, na Israeli wote pamoja naye, nao wakapiga Libna;
30. Bwana akautia na mji huo pia pamoja na mfalme wake mkononi mwa Israeli; naye akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia ndani yake; naye akamtenda mfalme wake kama alivyomtenda huyo mfalme wa Yeriko.
31. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Libna, na Israeli wote pamoja naye, wakafika Lakishi, wakapanga marago mbele yake na kupigana nao;
32. Bwana akautia huo mji wa Lakishi mkononi mwa Israeli, naye akautwaa siku ya pili, akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake, sawasawa na hayo yote aliyoutenda Libna.
33. Wakati huo Horamu, mfalme wa Gezeri, akakwea ili kuusaidia Lakishi, lakini Yoshua akampiga yeye na watu wake, hata asimsazie hata mtu mmoja.
34. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Lakishi, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Egloni; nao wakapanga marago mbele yake, na kupigana nao;
35. siku iyo hiyo wakautwaa, nao wakaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake akawaangamiza kabisa siku hiyo, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia mji wa Lakishi.
36. Kisha Yoshua akakwea kutoka hapo Egloni, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Hebroni; nao wakapigana nao;
37. wakautwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake, na miji yake yote, na wote waliokuwamo ndani yake; hakumwacha aliyesalia hata mtu mmoja, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia huo mji wa Egloni; lakini akauangamiza kabisa, na wote pia waliokuwamo ndani yake.
38. Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata Debiri; nao wakapigana nao;
39. kisha akautwaa, na mfalme wake, na miji yake yote; nao wakawapiga kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia; kama alivyoufanyia Hebroni aliufanyia na Debiri vivyo, na mfalme wake; kama alivyoufanyia Libna, na mfalme wake.
40. Basi Yoshua akaipiga nchi hiyo yote, nchi ya vilima, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela, na nchi ya matelemko, na wafalme wake wote; hakumwacha aliyesalia hata mmoja; lakini akawaharibu kabisa wote waliokuwa wavuta pumzi, kama Bwana, Mungu wa Israeli, alivyoamuru.
41. Yoshua akawapiga kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na nchi yote ya Gosheni, hata Gibeoni.
42. Na wafalme hao wote na nchi zao Yoshua akatwaa, wakati huo, kwa sababu yeye Bwana, Mungu wa Israeli, alipigana kwa ajili ya Israeli,
43. Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata marago yao huko Gilgali.

  Joshua (10/24)