| ← Jonah (3/4) → |
| 1. | Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, |
| 2. | Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru. |
| 3. | Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu. |
| 4. | Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. |
| 5. | Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. |
| 6. | Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. |
| 7. | Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; |
| 8. | bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. |
| 9. | Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? |
| 10. | Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende. |
| ← Jonah (3/4) → |