Jonah (2/4)  

1. Ndipo Yona akamwomba Bwana, Mungu wake, katika tumbo la yule samaki,
2. Akasema, Nalimlilia Bwana kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu.
3. Maana ulinitupa vilindini, Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji ikanizunguka pande zote; Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu.
4. Nami nikasema, Nimetupwa mbali na macho yako; Lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu.
5. Maji yalinizunguka, hata nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga kichwa changu;
6. Nalishuka hata pande za chini za milima; Hiyo nchi na mapingo yake yalinifunga hata milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu kutoka shimoni, Ee Bwana, Mungu wangu,
7. Roho yangu ilipozimia ndani yangu, Nalimkumbuka Bwana; Maombi yangu yakakuwasilia, Katika hekalu lako takatifu.
8. Watu waangaliao mambo ya ubatili na uongo Hujitenga na rehema zao wenyewe;
9. Lakini mimi nitakutolea sadaka kwa sauti ya shukrani; Nitaziondoa nadhiri zangu. Wokovu hutoka kwa Bwana.
10. Bwana akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.

  Jonah (2/4)