Jonah (1/4)  

1. Basi neno la Bwana lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,
2. Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.
3. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa Bwana; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa Bwana.
4. Lakini Bwana alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.
5. Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.
6. Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.
7. Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.
8. Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani?
9. Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.
10. Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa Bwana, kwa sababu alikuwa amewajulisha.
11. Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka.
12. Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata.
13. Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana.
14. Basi wakamlilia Bwana, wakasema, Twakuomba, Ee Bwana, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, Bwana, umefanya kama ulivyopenda.
15. Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka.
16. Ndipo wale watu wakamwogopa Bwana mno, wakamtolea Bwana sadaka, na kuweka nadhiri.
17. Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.

      Jonah (1/4)