← John (16/21) → |
1. | Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. |
2. | Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. |
3. | Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. |
4. | Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi. |
5. | Lakini sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi? |
6. | Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu. |
7. | Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. |
8. | Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. |
9. | Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; |
10. | kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena; |
11. | kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa. |
12. | Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. |
13. | Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. |
14. | Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. |
15. | Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari. |
16. | Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona. |
17. | Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? Na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba? |
18. | Basi walisema, Neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo? Hatujui asemalo. |
19. | Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? |
20. | Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. |
21. | Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni. |
22. | Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye. |
23. | Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. |
24. | Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. |
25. | Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambapo sitasema nanyi tena kwa mithali, lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba. |
26. | Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; |
27. | kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba. |
28. | Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba. |
29. | Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote. |
30. | Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote, wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu. |
31. | Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa? |
32. | Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. |
33. | Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu. |
← John (16/21) → |