← John (15/21) → |
1. | Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. |
2. | Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. |
3. | Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. |
4. | Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. |
5. | Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. |
6. | Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. |
7. | Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. |
8. | Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu. |
9. | Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. |
10. | Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. |
11. | Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. |
12. | Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. |
13. | Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. |
14. | Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. |
15. | Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. |
16. | Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. |
17. | Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana. |
18. | Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. |
19. | Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. |
20. | Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. |
21. | Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka. |
22. | Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi yao. |
23. | Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu. |
24. | Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia. |
25. | Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure. |
26. | Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. |
27. | Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami. |
← John (15/21) → |