| ← John (14/21) → | 
| 1. | Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. | 
| 2. | Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. | 
| 3. | Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. | 
| 4. | Nami niendako mwaijua njia. | 
| 5. | Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? | 
| 6. | Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. | 
| 7. | Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. | 
| 8. | Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. | 
| 9. | Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? | 
| 10. | Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. | 
| 11. | Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. | 
| 12. | Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. | 
| 13. | Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. | 
| 14. | Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. | 
| 15. | Mkinipenda, mtazishika amri zangu. | 
| 16. | Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; | 
| 17. | ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. | 
| 18. | Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. | 
| 19. | Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. | 
| 20. | Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. | 
| 21. | Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. | 
| 22. | Yuda (siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? | 
| 23. | Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. | 
| 24. | Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. | 
| 25. | Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. | 
| 26. | Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. | 
| 27. | Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. | 
| 28. | Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. | 
| 29. | Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. | 
| 30. | Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. | 
| 31. | Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu. | 
| ← John (14/21) → |