| ← John (12/21) → |
| 1. | Basi, siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu. |
| 2. | Basi wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumikia; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye. |
| 3. | Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu. |
| 4. | Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, |
| 5. | Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? |
| 6. | Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo. |
| 7. | Basi Yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu. |
| 8. | Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamnami sikuzote. |
| 9. | Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika wafu. |
| 10. | Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye; |
| 11. | maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu. |
| 12. | Nayo siku ya pili yake watu wengi walioijia sikukuu walisikia ya kwamba Yesu anakuja Yerusalemu; |
| 13. | wakatwaa matawi ya mitende, wakatoka nje kwenda kumlaki, wakapiga makelele, Hosana! Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli! |
| 14. | Naye Yesu alikuwa amepata mwana-punda, akampanda, kama vile iliyoandikwa, |
| 15. | Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda. |
| 16. | Mambo hayo wanafunzi wake hawakuyafahamu hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kwamba ameandikiwa hayo, na ya kwamba walimtendea hayo. |
| 17. | Basi wakamshuhudia wale mkutano waliokuwapo pamoja naye alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua. |
| 18. | Na kwa sababu hiyo mkutano walikwenda kumlaki, kwa kuwa wamesikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo. |
| 19. | Basi Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, Mwaona kwamba hamfai neno lo lote; tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake. |
| 20. | Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu. |
| 21. | Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu. |
| 22. | Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu. |
| 23. | Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. |
| 24. | Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. |
| 25. | Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. |
| 26. | Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. |
| 27. | Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. |
| 28. | Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena. |
| 29. | Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye. |
| 30. | Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. |
| 31. | Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. |
| 32. | Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu. |
| 33. | Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa. |
| 34. | Basi mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana wa Adamu ni nani? |
| 35. | Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako. |
| 36. | Maadamu mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru. Hayo aliyasema Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone. |
| 37. | Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini; |
| 38. | ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? |
| 39. | Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena, |
| 40. | Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. |
| 41. | Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake. |
| 42. | Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. |
| 43. | Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu. |
| 44. | Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. |
| 45. | Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. |
| 46. | Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. |
| 47. | Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. |
| 48. | Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. |
| 49. | Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. |
| 50. | Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo. |
| ← John (12/21) → |