Job (9/42)  

1. Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2. Kweli najua kuwa ndivyo hivyo; Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?
3. Kama akipenda kushindana naye, Hawezi kumjibu neno moja katika elfu.
4. Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu; Ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?
5. Aiondoaye milima, nayo haina habari, Akiipindua katika hasira zake.
6. Aitikisaye dunia itoke mahali pake, Na nguzo zake hutetema.
7. Aliamuruye jua, nalo halichomozi; Nazo nyota huzipiga muhuri.
8. Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu, Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.
9. Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia, Na makundi ya nyota ya kusini.
10. Atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; Naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika.
11. Tazama, yuaenenda karibu nami, nisimwone; Tena yuapita kwenda mbele, nisimtambue.
12. Tazama, yuakamata, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini?
13. Mungu haondoi hasira zake; Hao wamsaidiao Rahabu huinama chini yake.
14. Je! Mimi nitamjibuje, Na kuyachagua maneno yangu kuhojiana naye?
15. Ambaye, nijapokuwa mimi ni mwenye haki, nisingemjibu; Ningemsihi-sihi mtesi wangu.
16. Kama ningemwita, naye akaniitikia; Hata hivyo singeamini kuwa amesikiza sauti yangu.
17. Yeye anipondaye kwa dhoruba, Na kuziongeza jeraha zangu pasipokuwa na sababu.
18. Haniachi nipate kuvuta pumzi, Lakini hunijaza uchungu.
19. Kama tukitaja nguvu za mashujaa, tazama yupo hapo! Kama tukitaja hukumu, ni nani atakayeniwekea muhula?
20. Ingawa ni mwenye haki, kinywa changu mwenyewe kitanihukumu; Ingawa ni mkamilifu, kitanishuhudia kuwa ni mpotovu.
21. Mimi ni mkamilifu; siangalii nafsi yangu; Naudharau uhai wangu.
22. Hayo yote ni mamoja; kwa hiyo nasema, Yeye huangamiza wakamilifu na waovu pia.
23. Kama hilo pigo likiua ghafula, Atayadhihaki majaribu yake asiye na kosa.
24. Dunia imetiwa mkononi mwa waovu; Yeye hufunika nyuso za waamuzi wake; Kama si yeye, ni nani basi?
25. Basi siku zangu zina mbio kuliko tarishi; Zakimbia, wala hazioni mema.
26. Zimepita kama merikebu ziendazo mbio; Mfano wa tai ayashukiaye mawindo.
27. Nikisema, Mimi nitasahau kuugua kwangu, Nitaacha kununa uso nikachangamke moyo;
28. Mimi huziogopa huzuni zangu zote, Najua kuwa hutanihesabu kuwa sina hatia.
29. Nitahukumiwa kuwa ni mkosa; Ya nini basi nitaabike bure?
30. Ingawaje najiosha kwa maji ya theluji, Na kuitakasa mikono yangu kwa sabuni;
31. Lakini utanitupa shimoni, Nami hata nguo zangu zitanichukia.
32. Kwani yeye si mtu, kama mimi, hata nimjibu, Hata tukaribiane katika hukumu.
33. Hapana mwenye kuamua katikati yetu, Awezaye kutuwekea mkono sote wawili.
34. Na aniondolee fimbo yake, Na utisho wake usinitie hofu;
35. Ndipo hapo ningesema, nisimwogope; Kwani sivyo nilivyo nafsini mwangu.

  Job (9/42)