Job (8/42)  

1. Ndipo Bildadi huyo Mshuhi akajibu, na kusema,
2. Wewe utanena maneno haya hata lini? Maneno ya kinywa chako yatakuwa kama upepo mkuu hata lini?
3. Je! Mungu hupotosha hukumu? Au, huyo Mwenyezi hupotosha yaliyo ya haki?
4. Kwamba watoto wako wamemfanyia dhambi, Naye amewatia mkononi mwa kosa lao;
5. Wewe ukimtafuta Mungu kwa bidii, Na kumsihi huyo Mwenyezi;
6. Ukiwa wewe u safi na mwelekevu; Hakika yeye sasa angeamka kwa ajili yako, Na kuyafanya makazi ya haki yako kufanikiwa.
7. Tena ujapokuwa huo mwanzo wako ulikuwa ni mdogo, Lakini mwisho wako ungeongezeka sana.
8. Basi, uwaulize, tafadhali, vizazi vya zamani, Ujitie kuyaangalia yale baba zao waliyoyatafuta;
9. (Kwani sisi tu wa jana tu, wala hatujui neno, Kwa kuwa siku zetu duniani ni kivuli tu;)
10. Je! Hawatakufunza wao, na kukueleza, Na kutamka maneno yatokayo mioyoni mwao?
11. Je! Hayo mafunjo yamea pasipo matope Na makangaga kumea pasipo maji?
12. Yakiwa yakali mabichi bado, wala hayakukatwa, Hunyauka mbele ya majani mengine.
13. Ndivyo ulivyo mwisho wa hao wamsahauo Mungu; Na matumaini yake huyo mbaya huangamia;
14. Uthabiti wake utavunjika, Na matumaini yake huwa ni nyuzi za buibui.
15. Ataitegemea nyumba yake, isisimame; Atashikamana nayo, isidumu.
16. Yeye huwa mti mbichi mbele ya jua, Nayo machipukizi yake huenea katika bustani yake.
17. Mizizi yake huzonga-zonga chuguu, Huangalia mahali penye mawe.
18. Lakini, aking'olewa mahali pake, Ndipo patamkana, na kusema, Mimi sikukuona.
19. Tazama, furaha ya njia yake ni hii, Na wengine watachipuka kutoka katika nchi.
20. Tazama, Mungu hatamtupa mtu mkamilifu, Wala hatawathibitisha watendao uovu.
21. Bado atakijaza kinywa chako kicheko, Na midomo yako ataijaza shangwe.
22. Hao wakuchukiao watavikwa aibu; Nayo hema yake mwovu haitakuwako tena.

  Job (8/42)