| ← Job (7/42) → |
| 1. | Je! Mtu hana wakati wake wa vita juu ya nchi? Na siku zake, je! Si kama siku za mwajiriwa? |
| 2. | Kama mtumishi atamaniye sana kile kivuli, Kama mwajiriwa anayetazamia mshahara wake; |
| 3. | Ni vivyo nami nimepewa miezi ya ubatili iwe fungu langu, Nami nimeandikiwa masiku yenye kuchokesha. |
| 4. | Hapo nilalapo chini, nasema, Nitaondoka lini? Lakini usiku huwa mrefu; Nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke. |
| 5. | Mwili wangu unavikwa mabuu na madongoa ya udongo; Ngozi yangu hufumba, kisha ikatumbuka tena. |
| 6. | Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia, Nazo zapita pasipokuwa na matumaini. |
| 7. | Kumbuka ya kwamba maisha yangu ni upepo; Jicho langu halitaona mema tena. |
| 8. | Jicho lake huyo anionaye halitaniangalia tena; Macho yako yatanielekea, lakini sitakuwapo. |
| 9. | Kama vile wingu likomavyo na kutoweka, Ni vivyo huyo ashukaye kuzimuni hatazuka tena kabisa. |
| 10. | Hatarudi tena nyumbani kwake, Wala mahali pake hapatamjua tena. |
| 11. | Kwa hiyo sitakizuia kinywa changu; Nitanena kwa mateso ya roho yangu; Nitalia kwa uchungu wa nafsi yangu. |
| 12. | Je! Mimi ni bahari, au je! Ni nyangumi? Hata ukawaweka walinzi juu yangu? |
| 13. | Hapo nisemapo, kitanda changu kitanituza moyo, Malazi yangu yatanipunguzia kuugua kwangu; |
| 14. | Ndipo unitishapo kwa ndoto, Na kunitia hofu kwa maono; |
| 15. | Hata nafsi yangu huchagua kunyongwa, Na kuchagua kifo kuliko maumivu yangu haya. |
| 16. | Ninadhoofika; sitaishi sikuzote; Usinisumbue, kwani siku zangu ni uvuvio. |
| 17. | Je! Mtu ni kitu gani, hata ukamtukuza, Na kumtia moyoni mwako, |
| 18. | Na kumwangalia kila asubuhi, Na kumjaribu kila dakika? |
| 19. | Je! Hata lini hukomi kuniangalia; Wala kunisumbua hata nimeze mate? |
| 20. | Kwamba nimefanya dhambi, nikufanyieje Ee mlinda wanadamu? Mbona umeniweka niwe shabaha yako, Hata nimekuwa mzigo kwa nafsi yangu? |
| 21. | Nawe, je! Mbona hunisamehe makosa yangu, Na kuniondolea maovu yangu? Kwa kuwa sasa nitalala mavumbini; Nawe utanitafuta kwa bidii, lakini sitakuwapo. |
| ← Job (7/42) → |