| ← Job (6/42) → |
| 1. | Ndipo Ayubu akajibu na kusema, |
| 2. | Laiti uchungu wangu ungepimwa, Na msiba wangu kutiwa katika mizani pamoja! |
| 3. | Kwa kuwa sasa ungekuwa mzito kuliko mchanga wa bahari; Kwa hiyo maneno yangu yamekuwa ya haraka. |
| 4. | Kwa kuwa mishale ya huyo Mwenyezi i ndani yangu, Na roho yangu inainywa sumu yake; Vitisho vya Mungu vimejipanga juu yangu. |
| 5. | Je! Huyo punda-mwitu hulia akiwa na majani? Au, ng'ombe hulia malishoni? |
| 6. | Je! Kitu kisicho na ladha yumkini kulika pasipo chumvi? Au je, uto wa yai una tamu iwayo yote? |
| 7. | Roho yangu inakataa hata kuvigusa; Kwangu mimi ni kama chakula kichukizacho. |
| 8. | Laiti ningepewa haja yangu, Naye Mungu angenipa neno hilo ninalolitamani sana! |
| 9. | Kwamba Mungu angekuwa radhi kuniseta; Kwamba angeulegeza mkono wake na kunikatilia mbali! |
| 10. | Hapo ndipo ningefarijika hata sasa; Naam, ningejikuza katika maumivu yasiyoniacha; Kwa kuwa sikuyakana maneno yake Mtakatifu. |
| 11. | Nguvu zangu ni zipi, hata ningoje? Na mwisho wangu ni nini, hata nisubiri? |
| 12. | Je! Nguvu zangu ni nguvu za mawe? Au mwili wangu, je! Ni shaba? |
| 13. | Je! Si kwamba sina msaada ndani yangu. Tena kwamba kufanikiwa kumeondolewa mbali nami? |
| 14. | Kwake huyo atakaye kuzima roho inapasa atendewe mema na rafiki; Hata kwake huyo aachaye kumcha Mwenyezi. |
| 15. | Ndugu zangu wametenda udanganyifu kama kijito cha maji. Mfano wa fumbi la vijito vipitavyo. |
| 16. | Vilivyokuwa vyeusi kwa sababu ya barafu, Ambamo theluji hujificha. |
| 17. | Wakati vipatapo moto hutoweka; Kukiwako hari, hukoma mahali pao. |
| 18. | Misafara isafiriyo kwa njia yao hugeuka; Hukwea kwenda barani, na kupotea. |
| 19. | Misafara ya Tema huvitazama, Majeshi ya Sheba huvingojea. |
| 20. | Wametahayari kwa sababu walitumaini; Wakaja huku, nao walifadhaika. |
| 21. | Kwani sasa ninyi mmekuwa vivyo; Mwaona jambo la kutisha, mkaogopa. |
| 22. | Je! Nilisema, Nipeni? Au, Nitoleeni toleo katika mali yenu? |
| 23. | Au, Niokoeni na mkono wa adui? Au, Nikomboeni na mikono ya hao waoneao? |
| 24. | Nifunzeni, nami nitanyamaa kimya; Mkanijulishe ni jambo gani nililokosa. |
| 25. | Jinsi yafaavyo maneno ya uelekevu! Lakini kuhoji kwenu, je! Kumeonya nini? |
| 26. | Je! Mwafikiri kuyakemea maneno? Maana maneno ya huyo aliyekata tamaa ni kama upepo. |
| 27. | Naam, mwapenda kuwapigia kura hao mayatima, Na kufanya biashara ya rafiki yenu. |
| 28. | Sasa basi iweni radhi kuniangalia; Kwani hakika sitanena uongo usoni penu. |
| 29. | Rudini, nawasihi, lisiwe neno la udhalimu; Naam, rudini tena, neno langu ni la haki. |
| 30. | Je! Mna udhalimu ulimini mwangu? Je! Makaakaa yangu hayatambui mambo ya madhara? |
| ← Job (6/42) → |