| ← Job (5/42) → |
| 1. | Haya, ita sasa; je! Yuko atakayekujibu? Nawe utamwelekea yupi katika hao watakatifu? |
| 2. | Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga. |
| 3. | Nimewaona wapumbavu wakishusha mizizi; Lakini mara niliyalaani maskani yake. |
| 4. | Watoto wake wako mbali na wokovu, Nao wamesongwa langoni, Wala hapana atakayewaponya. |
| 5. | Mavuno yake wale wenye njaa huyala, Na kuyatwaa hata kuyatoa miibani, Nao wenye kiu huzitwetea mali zao. |
| 6. | Kwani taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi; |
| 7. | Lakini mwanadamu huzaliwa ili apate mashaka, Kama cheche za moto zirukavyo juu. |
| 8. | Lakini mimi ningemtafuta Mungu, Ningemwekea Mungu daawa yangu; |
| 9. | Yeye afanyaye mambo makuu, yasiyotambulikana; Mambo ya ajabu yasiyo na hesabu; |
| 10. | Yeye atoaye mvua inyeshe juu ya nchi, Na kuyapeleka maji mashambani; |
| 11. | Awainuaye juu hao walio chini; Na hao waombolezao hukuzwa wawe salama. |
| 12. | Yeye huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao. |
| 13. | Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao wenyewe; Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka. |
| 14. | Wao hupatwa na giza wakati wa mchana, Hupapasa mchana vilevile kama usiku. |
| 15. | Lakini yeye huokoa na upanga wa kinywa chao, Hata kumwokoa mhitaji na mkono wake aliye hodari. |
| 16. | Basi hivi huyo maskini ana matumaini, Na uovu hufumba kinywa chake. |
| 17. | Tazama, yu heri mtu yule Mungu amwadhibuye; Kwa hiyo usidharau kurudiwa na huyo Mwenyezi. |
| 18. | Kwani yeye huumiza, lakini tena huuguza; Yeye hutia jeraha, na mikono yake huponya. |
| 19. | Yeye atakuokoa na mateso sita; Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa. |
| 20. | Wakati wa njaa atakukomboa na mauti; Na vitani atakukomboa na nguvu za upanga. |
| 21. | Utafichwa na mapigo ya ulimi; Wala usiogope maangamizo yatakapokuja. |
| 22. | Wewe utayacheka maangamizo na njaa; Wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi. |
| 23. | Kwani utakuwa na mapatano na mawe ya bara; Nao wanyama wa bara watakuwa na amani kwako. |
| 24. | Nawe utajua ya kwamba hema yako ina salama; Na zizi lako utaliaua, wala usikose kitu. |
| 25. | Tena utajua ya kwamba uzao wako utakuwa mwingi, Na vizazi vyako watakuwa kama nyasi za nchi. |
| 26. | Utafika kaburini mwenye umri mtimilifu, Kama mganda wa ngano ulivyo wakati wake. |
| 27. | Tazama, haya tumeyapeleleza, ndivyo yalivyo; Yasikie, uyajue, ili upate mema. |
| ← Job (5/42) → |