| ← Job (41/42) → |
| 1. | Je! Waweza wewe kumvua mamba kwa ndoana? Au, kuufunga ulimi wake kwa kamba? |
| 2. | Je! Waweza kutia kamba puani mwake? Au kutoboa taya yake kwa kulabu? |
| 3. | Je! Atakusihi sana? Au, atakuambia maneno ya upole? |
| 4. | Je! Atafanya agano pamoja nawe, Umtwae kuwa mtumishi wako milele? |
| 5. | Je! Utamchezea kama ndege? Au, kumfunga kwa ajili ya wasichana wako? |
| 6. | Je! Vikosi vya wavuvi watamfanyia biashara? Watamgawanya kati ya wafanyao biashara? |
| 7. | Je! Waweza kuijaza ngozi yake na vyuma vyenye ncha, Au kichwa chake kwa vyusa? |
| 8. | Mwekee mkono wako; Vikumbuke vile vita, wala usifanye tena. |
| 9. | Tazama, kumtamani ni bure; Je! Hatambwaga chini huyo atakayemtazama? |
| 10. | Hapana aliye mkali hata akathubutu kumwamsha; Bali ni nani awezaye kusimama mbele yangu mimi? |
| 11. | Ni nani aliyetangulia kunipa hata nimlipe? Kila kilicho chini ya mbingu nzima ni changu. |
| 12. | Sitanyamaa kusema habari za via vyake, Wala nguvu zake kuu, wala umbo lake zuri. |
| 13. | Ni nani awezaye kumbambua magamba yake? Ni nani atakayepenya dirii yake maradufu? |
| 14. | Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake. |
| 15. | Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama kwa kufungwa kwa muhuri. |
| 16. | Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati. |
| 17. | Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezekani kutengwa. |
| 18. | Kwa kuchemua kwake mwanga humemetuka, Na macho yake yanafanana na makope ya alfajiri. |
| 19. | Mienge iwakayo hutoka kinywani mwake, Na macheche ya moto huruka nje. |
| 20. | Moshi hutoka katika mianzi ya pua yake, Kama nyungu ikitokota, na manyasi yawakayo. |
| 21. | Pumzi zake huwasha makaa, Na miali ya moto hutoka kinywani mwake. |
| 22. | Katika shingo yake hukaa nguvu, Na utisho hucheza mbele yake. |
| 23. | Manofu ya nyama yake hushikamana; Yanakazana juu yake; hayawezi kuondolewa. |
| 24. | Moyo wake una imara kama jiwe; Naam, imara kama jiwe la chini la kusagia. |
| 25. | Anapojiinua, mashujaa huogopa; Kwa sababu ya woga wao huvunjwa moyo. |
| 26. | Mtu akimpiga kwa upanga, haumwingii; Wala fumo, wala mshale, wala mkuki wenye ncha. |
| 27. | Yeye huona chuma kuwa kama nyasi, Na shaba kama mti uliooza. |
| 28. | Mshale hauwezi kumkimbiza; Na mawe ya teo kwake hugeuka kuwa kama makapi. |
| 29. | Marungu huhesabiwa kama mabua; Naye hucheka mshindo wa mkuki ukitupwa. |
| 30. | Pande zake za chini ni kama vigae vikali; Hutandika malazi kama kuweka chombo cha kupuria nafaka juu ya matope. |
| 31. | Yeye huchemsha kilindi mfano wa nyungu; Hufanya bahari kuwa kama mafuta. |
| 32. | Hufanya mapito yake kung'aa nyuma yake Hata mtu angedhani kilindi kina mvi. |
| 33. | Juu ya nchi hapana aliyefanana naye, Aliyeumbwa pasipo oga. |
| 34. | Yeye hutazama kila kitu kilicho juu; Ni mfalme juu ya wote wenye kiburi. |
| ← Job (41/42) → |