← Job (39/42) → |
1. | Je! Wajua majira ya kuzaa kwao mbuzi-mwitu walio majabalini? Au waweza kusema majira ya kuzaa kulungu? |
2. | Je! Waweza kuhesabu miezi yao watakayoitimiza? Au je! Wajua majira ya kuzaa kwao? |
3. | Wao hujiinamisha, kuzaa watoto wao, Watupa taabu zao. |
4. | Watoto wao wa katika hali nzuri, hukua katika bara wazi; Huenda zao, wala hawarudi tena. |
5. | Ni nani aliyempeleka punda-milia aende huru? Au je! Ni nani aliyemfungulia vifungo punda-mwitu? |
6. | Ambaye nimeifanya nyika kuwa nyumba yake, Na nchi ya chumvi kuwa makao yake. |
7. | Yeye hudharau mshindo wa mji, Wala hasikii kelele zake msimamizi. |
8. | Upana wa milima ni malisho yake, Hutafuta-tafuta kila kitu kilicho kibichi. |
9. | Je! Nyati atakubali kukutumikia? Au atakaa katika zizi lako? |
10. | Je! Waweza kumfunga nyati kwa kamba matutani? Au, yeye atayalima mabonde nyuma yako? |
11. | Je! Utamtumaini kwa sababu ana nguvu nyingi? Au, utamwachia yeye kazi yako? |
12. | Je! Utamtumaini kwamba ataileta mbegu yako nyumbani. Na kukusanya nafaka ya kiwanja chako cha kupuria? |
13. | Bawa la mbuni hufurahi; Lakini mabawa yake na manyoya yake, je! Yana huruma? |
14. | Kwani yeye huyaacha mayai yake juu ya nchi, Na kuyatia moto mchangani, |
15. | Na kusahau kwamba yumkini mguu kuyavunja, Au mnyama wa mwitu kuyakanyaga. |
16. | yeye huyafanyia ukali makinda yake, kana kwamba si yake; Ijapokuwa taabu yake ni ya bure, hana hofu; |
17. | Kwa sababu Mungu amemnyima akili, Wala hakumpa fahamu. |
18. | Wakati anapojiinua juu aende, Humdharau farasi na mwenye kumpanda. |
19. | Je! Wewe ulimpa farasi uwezo wake? Au, ni wewe uliyemvika shingo yake manyoya yatetemayo? |
20. | Ndiwe uliyemfanya aruke kama nzige? Fahari ya mlio wake hutisha. |
21. | Hupara-para bondeni, na kuzifurahia nguvu zake; Hutoka kwenda kukutana na wenye silaha. |
22. | Yeye hufanyia kicho dhihaka, wala hashangai; Wala hageuki kurudi nyuma mbele ya upanga. |
23. | Podo humpigia makelele, Mkuki ung'aao na fumo. |
24. | Huimeza nchi kwa ukali wake na ghadhabu; Wala hasimami kwa sauti ya baragumu. |
25. | Kila ipigwapo baragumu yeye husema, Aha! Naye husikia harufu ya vita toka mbali, Mshindo wa maakida, na makelele. |
26. | Je! Mwewe huruka juu kwa akili zako, Na kuyanyosha mabawa yake kwenda kusini? |
27. | Je! Tai hupaa juu kwa amri yako, Na kufanya kioto chake mahali pa juu? |
28. | Hukaa jabalini, ndiko kwenye malazi yake, Juu ya genge la jabali, na ngomeni. |
29. | Toka huko yeye huchungulia mawindo; Macho yake huyaangalia toka mbali. |
30. | Makinda yake nayo hufyonza damu; Na kwenye maiti ndiko aliko. |
← Job (39/42) → |